BEI YA DIZELI YASHUKA SOMA UZIJUE SABABU ZA KUSHUKA
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA , Mhandisi Godfrey Chibulunje akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .
*****************************
Happy Lazaro,Arusha
Arusha.BEI ya mafuta ya Dizeli imeshuka kwa sh.18 katika Bandari ya Dar es Salamu kutoka Sh.2,261 kwa Lita mwezi Oktoba na kufikia Sh.2,243 kwa Lita moja mwezi huu, huku bei ya mafuta ya Petroli ikibaki hivyo hivyo.
Akitangaza kushuka kwa bei ya Dizeli leo Jijini Arusha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema mafuta hayo yameshuka kutokana jitihada za serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa bei nafuu licha ya soko la Dunia kupanda.
“Katika soko la Dunia bei zinazidi kupanda lakini serikali imefanya juhudi mbalimbali za kufuta tozo na imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na soko la dunia katika upandaji wa bei za mafuta hivyo serikali inajali wananchi wake,”amesema Chibulunje.
Amesema kuwa, bei hiyo ya mafuta ya Dizeli itaanza kutumika kesho (Jumatano) na kusisitiza bei ya Petroli kuwa hivyo hivyo kama awali ya Sh.2, 439 kwa lita moja.
Amesema bei ya mafuta ya taa katika bandari ya Dar es Salaam itaendelea kuwa Sh.2,188 kwa lita moja na katika bandari ya Tanga bei ya mafuta ya petroli ilikuwa ni Sh.2,478 kwa lita moja huku Dizeli ilikuwa inauzwa Sh.2,245 kwa lita moja na zitaendelea kubaki hivyo hivyo.
Alisema katika bandari ya Mtwara bei ya mafuta itabaki kama ilivyo ambapo petroli itakuwa ni Sh.2,455 na Dizeli Sh.2,279 huku bei ya mafuta ya taa ikiwa ni Sh.2,260 kwa lita moja.
Amesisitiza bei ya mafuta ya Petroli itakabaki hivyo hivyo na serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kudhibiti upandaji wa bei za bidhaa hizo.
Ameongeza kuwa, bei hiyo katika soko la dunia imezidi kupanda ambapo Mei mwaka jana bei ya pipa moja la mafuta ghafi ilikuwa ni dola 32 hadi kufikia Oktoba 2021 katika soko la dunia mafuta hayo yalifikia dola 86 kwa pipa moja,hivyo bei zinazidi kupanda.
Post a Comment