Ads

Staa wa zamani wa Timu ya Taifa ya Ufaransa na club ya PSG Jean Pierre Adams amefariki Dunia

 



BEKI wa zamani wa Ufaransa, Jean-Pierre Adams, ambaye amekuwa kwenye koma kwa miaka 39, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 73, leo Jumatatu.

Adams alipelekwa hospitali Machi 1982 kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa goti, hakuweza kuamka tangu wakati huo baada ya kufanyika makosa kwenye upasuaji wake.

Akiwa mzaliwa wa Senegal, beki huyo alicheza zaidi ya mechi 140 kwenye kikosi cha Nice na aliwahi kuitumikia Paris Saint Germain.

Klabu ya Nice ilisema kwamba itatoa heshima yake kwa Adams, ambaye aliichezea timu ya taifa ya Ufaransa mechi 22 kati ya mwaka 1972 na 1976  wakati wa mechi yao ijayo ya ligi dhidi ya Monaco, Septemba 19. Adams aliichezea pia mechi 84 klabu ya Nimes, ambayo imetuma rambirambi zake kwa familia ya staa huyo wa zamani wa Les Bleus.

Katika siku ambayo Adams alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha msuli mkubwa wa goti, ambao aliumia mazoezini, madaktari wengi kwenye hospitali ya Lyon walikuwa kwenye mgomo.

Upasuaji ulifanyika, huku madaktari mmoja alikuwa na kazi ya kuhudumia wagonjwa wanane ndani ya muda mmoja, akiwamo Adams.
Adams alihudumiwa na mwanafunzi, ambaye baadaye alisema: "Sikuwa na ufahamu wa kazi niliyotakiwa nifanye."

Kutokana na hilo, makosa mengi yalifanyika na kusababisha Adams kupata shambulio la moyo ambayo iliathiri kwa kiwango kikubwa ubongo wake. Katikati ya miaka 1990, waliohusika na tukio walipewa adhabu ya kufungwa jela mwezi moja na faini ya Euro 750.

Adams aliruhusiwa kutoka hospitali baada ya miezi 15 na tangu wakati huo alikuwa kwenye koma huko nyumbani kwake, Nimes akihudumiwa na mkewe, mrembo Bernadette kabla ya umauti kumkukuta.

Bernadette Adams ni mwanamke mwenye upendo mkubwa, ambaye hakumpa kisogo mumewe na wala hakuwahi kuwaza kumzimia mashine ya kumsaidia kupumua licha ya kuwa kwenye hali ya hovyo.

Kwa karibu miongo minne, Bernadette amekuwa akimhudumia Jean-Pierre, kumbadilisha nguo, kumlisha chakula na amekuwa habanduki nyumbani ikiwamo kumwongelesha mtu ambaye alikuwa kwenye koma na hajielewi kwa chochote.
kutoka Mwananchi

No comments