Ads

RITA YAVUNJA REKODI YASAJILI VYETI VYA KUZALIWA KWA WANANCHI 10,495.

 

Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umevunja  rekodi ya kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi takribani 10,495 ndani ya siku 16 katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama SabaSaba.

Akitoa taarifa hiyo kutoka katika banda la RITA viwanja vya SabaSaba, Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Emmy Hudson amesema kuwa safari hii wananchi wengi wameonesha kuwa na muitikio mkubwa wa kufuatilia vyeti vya kuzaliwa na hii ni kutokana na kujua umuhimu wa kuwa na cheti hicho ili kujipatia mahitaji muhimu katika jamii yetu.

 Aidha, wananchi wameipongeza RITA kwa huduma ambayo wameitoa katika maonesho hayo bila ubaguzi wowote na bila usumbufu ambapo kila aliyehitaji huduma ya cheti cha kuzaliwa alipewa.

 Hudson amesema hayo mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi waliofika katika banda la RITA kwa ajili ya kupata vyeti vya kuzaliwa siku ya kufungwa kwa maonesho hayo, ambapo  yalifungwa rasmi na  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

 Amesema hatua hiyo, ni sehemu ya mkakati wa RITA kuwafikia wananchi katika kila sehemu na kutoa huduma pamoja na kwenye maadhimisho na maonesho mbalimbali kama hayo ili kuwarahisishia upatikanaji wake karibu na maeneo wanayoishi.

Hudson amesema licha ya maonesho hayo kumalizika bado wataendelea kutoa huduma hiyo katika ofisi  za RITA kama kawaida  hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kufika katika ofis za RITA ili kupata vyeti vya kuzaliwa kwani ni haki ya kila mtanzania kuwa na cheti hicho.

Pia, amesema RITA iko imara kwa kutoa huduma hiyo, kwasababu changamoto waliyoipata katika maonesho hayo ni watu kuwa wengi ambapo hatahivyo waliweza kuhakikisha kuwa kila aliyefika katika banda la RITA alipata huduma stahiki.

"Changamoto tuliyoipata ni watu kuwa wengi, ambapo ikasababisha huduma hiyo kutolewa hadi saa moja usiku, ili kila aliyefika katika banda hili aweze kupata huduma kulingana na mahitaji yake," Alisema Bi. Hudson.

Mmoja wa wananchi hao aliyejulikana kwa jina la Bi.Amina Abdallah ameipongeza RITA kwa huduma ambayo wameitoa na yeye kuweza kufanikiwa kupata cheti chake cha kuzaliwa kwa gharama nafuu na kwa haraka.

Amesema "kwakweli wananchi tulikuwa wengi sana ambao tunahitaji huduma ya vyeti, lakini tulipokelewa vizuri na maafisa wa RITA  waliokuwa wanatoa huduma na kutuhudumia kulingana na mahitaji yetu,naipongeza sana RITA kwa kutuletea huduma hii kwenye maonesho haya makubwa"

 Naye, Bwana Joseph Mashaka amesema kuwa, hakuwahi kutegemea kupata cheti cha kuzaliwa kulingana na umri wake kutokana na baadhi ya wananchi huko mtaani kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu ugumu wa  kupata huduma hiyo, lakini mara baada ya kufika katika banda hilo alipewa maelekezo na kisha kuanza hatua za kupata cheti tofauti na alivyodhani hapo awali.

 "Tunashukuru kupata huduma hii hapa hapa sabasaba, Mimi ni mkazi wa Chanika kwangu ilikuwa rahisi kufika hapa kwa sababu kila nilipotamani kuifuata huduma hii katika ofisi zao nilikuwa naona uvivu kwa kuona  kuwa ni mbali," amesema Mashaka

 Mmoja wa viongozi waliotembelea banda hilo ni Meya wa Jiji la Ilala, Mhe. Omary Kumbilamoto ambapo aliupongeza Wakala kwa kutoa huduma hiyo hadi muda wa usiku kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya cheti cha kuzaliwa.

"Kazi nzuri sana mnafanya, mmejitolea kufanya kazi hadi usiku ili wananchi waweze kupata vyeti vyao kwa kufuata utaratibu, msiishie hapa tu endeleeni kupeleka huduma hii karibu na jamii," amesema Kumbilamoto.

Maonesho hayo ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama SabaSaba yalifungwa rasmi tarehe 13 Julai  ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla.Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Emmy Hudson akizungumza na wananchi katika  banda la RITA wakati  maonesho 45 ya Biashara ya Kimataifa  ya Sabasaba yaliyofanyika mwezi huu kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere  Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.Afisa Mawasiliano  wa (RITA) Jafari Malema (kushoto) akizungumza na wananchi na waliofika kwenye banda la RITA  katika  maonesho 45 ya Biashara ya Kimataifa  ya Sabasaba yaliyofanyika mwezi huu kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere  Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka Michuzi TV) kushoto Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA),Emmy Hudson.Msajili Mwandamizi kutoka RITA, Rehema Mushi wakwanza kulia akiwa pamoja na maafiza wenzake wakiwahudumia wananchi waliofika kwenye banda la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) katika maonesho 45 ya Biashara ya Kimataifa  ya Sabasaba yaliyofanyika mwezi huu kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere  Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.


Kama inavyoonekana pichani  Maafisa wa RITA wakiendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi.
Wananchi wakiwa kwenye banda la RITA

No comments