Ads

MBUNGE MHE. MASSARE AKUTANA NA WANANCHI KUJADILI MAENDELEO YA KIJIJI

 Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi Mhe. Yahaya Omary Massare (katikati) akizungumza na wananchi wa Kijiji Cha Damwelu Kata ya Ipande Wilaya Ya Manyoni Mkoani Singida

NA AISHA MBEGU, SINGIDA

Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi Mhe.Yahaya Omary Massare amesema kuwa atachangia ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Damwelu Kata ya Ipande Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida endapo wananchi wa kijiji hicho watajitolea  kuanzisha ujenzi  huo.      

Akizungumza na Wanakijiji wa Damwelu Mbunge Mhe. Massare  amewashukuru kwa kumpigia kura za kutosha  pamoja na kueleza mikakati iliyopo na iliyotekelezwa tangu alipochaguliwa mwaka 2020. 

Amewataka wanakijiji hao kushirikiana na uongozi wa kijiji katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuboresha miundombinu mbalimbali na huduma za kijamii.         

Akijibu kero ya umeme iliyoelezwa na Diwani wa Kata ya Ipande Bw. Kedmon Japhet Mpondo, amesema kuwa tayari amepokea fedha kwa ajili ya usambazaji umeme katika vijiji 15 na tayari Mkadharasi amepatikana na atatangazwa wiki ijayo na kuanza kazi rasmi. 

Mhe. Massare amewataka viongozi wa vijiji kushirikiana na wakala wa umeme vijijini REA watakapofika kuwaonyesha maeneo ya makazi ya watu kwa ajili ya kuweka nguzo ili kuhakikisha kuwa wananchi wa vijiji hivyo wanapata umeme pasipokuwa na changamoto yoyote.

Amewataka viongozi wa dini zote kushirikiana na viongozi wa kijiji cha Damwelu kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kujitokeza kwa wingi katika kushiriki zoezi la sensa mwaka 2022.

Diwani wa kata ya Ipande  Kedmon Japhet Mpondo amemuomba mbunge huyo kuwasaidia katika kuboresha elimu katika kata hiyo jambo ambalo limejibiwa na Mbunge kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa kijiji cha Damwelu kinakuwa na shule Mbili za Msingi  ikiwemo kurasimishwa shule ya msingi Mgamboo kuwa shule kamili.

Katika mkutano huo ulihudhuriwa na wananchi wa kijiji cha Damwelu na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali kutoka katika kijiji na kata ya Ipande

No comments