BODI YA MAZIWA TANZANIA (TDB) ILIVYOTOA ELIMU KATIKA MAONESHO YA 45 YA BIASHARA YA KIMATAIFA SABASABA
Kaimu Meneja wa Masoko Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Bw. Michael Mkalati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Kaimu Meneja wa Masoko Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Bw. Michael Mkalati (akiwa upande wa kulia) akizungumza na wananchi waliotembelea Banda hilo katika maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Wananchi waliotembelea Banda la Bodi ya Maziwa Tanzania katika maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam wakipewa elimu na wafanyakazi wa TDB.
Picha ya kiwanda kidogo cha maziwa ambacho kinauwezo wa kuchakata maziwa lita 1,000 kwa siku.
....................
Wadau wametakiwa kuchangamkia fursa kwa kutembelea Banda la Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kwa ajili ya kupata elimu katika maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia ushiriki wa Bodi ya Maziwa Tanzania katika maonesho hayo, Kaimu Meneja wa Masoko, Bw. Michael Mkalati amesema kuwa wapo kwa ajili ya kuonesha kazi wanazotekeleza na kutoa elimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo majukumu ya kusimamia, kuendeleza, kuratibu pamoja na kuhamasisha matumizi na bidhaa zitokanazo na maziwa.
Bw. Mkalati amesema kuwa kunywaji wa maziwa ni muhimu sana kwa afya ya binadamu kutokana inaongeza virutubisho mwilini.
"Tupo kwa ajili kuelimisha jamii namna ya utumiaji wa maziwa pamoja na kuonesha fursa za kibiashara kwani mtu anapozalisha maziwa lita 100 ni sawa na kutoa ajira kwa watu wanne" amesema Bw. Mkalati.
Ameeleza kuwa katika sekta ya maziwa ni eneo muhimu, hivyo wadau watakapofika katika banda lao watapata taarifa itakayowasaidia kufanya uwekezaji wenye tija na kuongeza fursa katika soko la ajira.
Bw. Mkalati amefafanua kuwa kuna vitu mbalimbali ambavyo wamekuja kuonesha katika maonesho ya sabasaba ikiwemo kiwanda kidogo cha maziwa ambacho kinauwezo wa kuchakata maziwa lita 1,000 kwa siku.
Amesema kuwa kiwanda hicho ni rafiki kwa wafanyabishara wadogo kwa ajili ya kuchakata wa maziwa jambo ambalo litawasaidia kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.
"Tunatoa elimu namna ya kufuga, kufanya usafirishaji pamoja na watoa huduma mbalimbali wa maziwa" amesema Bw. Mkalati.
Amesema kuwa wadau wote watakaotembelea banda watapa elimu jinsi ya kupima na kutambua ubora wa maziwa ili mlaji aweze kutumia bidhaa iliyo bora.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa maziwa, amebainisha kuwa imegawanyika katika vipindi viwili ikiwemo kipindi cha kiangazi ambapo ni mwezi wa september upatikanaji wa waziwa ni changamoto, lakini katika kipindi cha mwezi wa Desemba hadi Machi maziwa yanakuwa mengi.
"Bodi inaendelea kuzifanyia kazi changamoto zote ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kwa maendeleo ya Taifa" amesema Bw. Mkalati.
Bodi ya Maziwa Tanzania imeundwa na sheria ya maziwa namba 8 ya mwaka 2004 ikiwa na majukumu ya kusimamia, kuendeleza, kuratibu pamoja na kuhamasisha matumizi ya maziwa na bidhaa zitokanazo na maziwa.
Post a Comment