MAJALIWA: TUMEPUNGUZA SIKU ZA KUSHUGHULIKIA MAOMBI YA VIBALI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema utaratibu wa utoaji wa vibali vya ukaazi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki umesaidia kupunguza hatua za kuchakata maombi kutoka siku 33 za hadi saba.
Amesema kuwa kwa sasa waombaji hawalazimiki kwenda katika Ofisi za Kazi kwa sababu taarifa zote zinapatikana kwenye mfumo na watajaza fomu moja tu ambayo huwa na taarifa zote za kazi na ukaazi tofauti na awali ambapo wawekezaji walilazimika kujaza fomu mbili.
Ameyasema hayo wakati akiahirisha mkutano wa tatu wa Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Agosti 31 mwaka huu.
Amesema miongoni mwa manufaa yaliyopatikana kupitia matumizi ya mfumo huo ni kupungua kwa siku za kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kutoka siku 14 hadi siku tatu. “Hali hii, pamoja na mambo mengine, imesaidia kupunguza malalamiko ya kuchelewa kupata majibu ya maombi ya vibali vya kazi.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kupokea maoni kutoka kwa watumiaji wa mfumo kwa ajili ya maboresho na tayari imeshakutana na kupokea maoni ya wadau wa ndani na nje kikiwemo Chama cha Wafanyakazi, Chama cha Waajiri (ATE), Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Taasisi ya Sekta Binafsi na kuyajumuisha maoni hayo kwenye maboresho.
Aidha Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo isimamie upatikanaji wa mbegu bora katika kilimo cha ngano na zabibu pamoja na kuweka mpango mzuri utakaosimamia na kuendeleza kilimo cha mazao hayo .
“…Utoaji wa vibali kwa wanunuzi wa ngano na mchuzi wa zabibu ufanywe kwa kuzingatia wale ambao watathibitisha kununua malighafi hizo ndani kwanza. Hakikisheni mnasimamia vizuri makubaliano kati ya wakulima na wanunuzi wakubwa ili tusinunue bidhaa hizo kutoka nje.”
Kuhusu kilimo cha mkataba, Waziri Mkuu amesema wameamua kutumia utaratibu huo kwa baadhi ya mazao yakiwemo ya alizeti, ngano, shayiri na soya ili kumpatia tija mkulima, ambapo kwa upande wa soya soko la uhakika lipo nchini China.
Post a Comment