Ads

WAZIRI MKUU MAJALIWA ,ATOA MAAGIZO MAZITO KWA MAMLAKA ZA UDHIBITI NCHINI

 


Mwamba wa habari

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameziagiza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, kufanya mabadiliko ya Kodi ili bidhaa zinazoingia zisitofautiane Bei na bidhaa zinazozalishwa nchini.

Aidha, Majaliwa ameziagiza mamlaka za udhibiti zihakikishe bidhaa zinazoingizwa nchini zinakuwa na ubora wa kimataifa huku bidhaa zisizo na viwango na bandia hazipati nafasi ya kuingia kwenye soko la Tanzania.

Majaliwa, ameyasema hayo  leo wakati wa kufungua Maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania katika Uwanja wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Bishara Tanzania (TANTRADE).

Maonyesho hayo yalibeba Kaulimbiu ya ‘Tumia Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania.’

Ameziagiza Wizara za Fedha na Mipango na Viwanda na Biashara ziendelee na mikakati ya kisera na kikodi ya namna ya kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nje na kuongeza ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa ndani ili kukuza viwanda vya ndani mfano; bidhaa za mbao, mafuta ya kula na saruji.

Amesema "Watanzania tuachane na fikra potofu kuwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi ndizo zenye ubora kuliko za hapa nchini, kwani bidhaa zetu ni bora na zina viwango vinavyostahili. Hebu sote tununue bidhaa zetu ili kukuza ajira na pato la mtu binafsi na Taifa kwa ujumla. Sisi Watanzania tunazalisha vitu bora na vyenye uhalisia,” amesema.

Amesema uwekezaji unaofanywa lazima uzingatie uendelevu, ubora na tija kulingana na viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa katika shughuli za uzalishaji ili kuhimili ushindani na hata kuweza kunufaika na fursa za masoko zinazoendelea kujitokeza. “Nina hakika tukijipanga tutaweza kuwa washindani mahiri na bidhaa zenu zitaingia na kuleta ushindani mkubwa kwenye soko.”

Majaliwa, aliwataka wawekezaji na wazalishaji wote nchini wafanye biashara halali, walipe kodi kikamilifu na wahakikishe wanatunza kumbukumbu vizuri ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi za biashara zinazofanyika ikiwemo na nchi jirani na kuweza kuandaa sera mahususi za kuwasaidia.

“Wizara ya Viwanda na Biashara hakikisheni wazalishaji wanatumia vizuri sheria za uasilia wa bidhaa ili kuweza kukidhi matakwa na kutumia fursa ya masoko ambayo Serikali yetu imesaini mikataba ya maridhiano hususani soko la Afrika Mashariki, SADC, AGOA na fursa nyingine za masoko ya pamoja,” alisema.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliagiza Halmashauri zote nchini zihakikishe viwanda vilivyo katika mamlaka zao vinashiriki kuonesha bidhaa wanazozalisha ili bidhaa hizo ziweze kutafutiwa masoko katika nchi mbalimbali duniani zikwemo nchi za Ukanda wa EAC na SADC kwa lengo la kuongeza mauzo ya Tanzania nje ya nchi.

“SIDO kwa kushirikiana na VETA wekeni kipaumbele cha kutoa mafunzo na kubuni nyenzo zinazoendana na mahitaji makubwa yaliyomo katika jamii ikiwemo katika eneo la kuchakata mazao kama korosho, chikichi, ufuta, alizeti na matumizi ya TEHAMA katika kuboresha uzalishaji mali, ufanisi, viwango na kutafuta masoko.”

Aliagiza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kufanya maboresho katika uratibu wa maonesho mbalimbali ya Viwanda na Biashara ili yafanyike kwa kuzingatia kanda za uzalishaji nchini badala ya nguvu kubwa kuelekezwa Dar Es Salaam na miji mikubwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Profesa Riziki Shemdoe, amesema katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Dk. Magufuli, viwanda vimeongezeka kufikia 8,477.

Naye Mkurugenzi wa TANTRADE Edwin Rutageruka, alisema maonyesho hayo yanafuatia agizo la Rais alilolitoa mwaka 2016 la kutaka kufanyika kwa maonyesho hayo.

Amese, maonyesho ya mwaka huu yamebana kauli mbiu ya 'Tumia bidhaa ya Tanzania, jenga uchumi wa Tanzania

No comments