UFUKWE WACHAFUKA , DC ILALA AONYA WANANCHI WAACHE KUTUPA TAKA MTONI
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng'wilabuzu Ludigija watatu mbele upande wa kushoto ,akishiriki zoezi la usafi maeneo ya ufuko wa Ocean road na Aga khan leo ,wakwaza mbele upande wa kushoto ni katibu tawala Wilaya ya Ilala Charangwa Makwiro na wakwanza upande wa kulia ni diwani wa kata ya Kivukoni Sharik Choughule
Baadhi ya watumishi wa Manispaa ya Ilala na Green west Pro na boda boda walijitokeza kushiriki zoezi la usafi wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija
Mwamba wa Habari
Wananchi wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam wametakiwa kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuepuka kutupa taka pembezoni mwa mto hususani msimbazi ili kutoviathiri viumbe vilivyo baharini.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng'wilabuzu Ludigija wakati akishiriki kwenye zoezi la usafi katika fukwe za bahari ya hindi katika maeneo ya Ocean Road pamoja na Agha Khan katika manispaa hiyo ikiwa ni kuunga mkono kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam aliyoitoa jumalilipita ambapo alizitaka Manispaa zote za mkoa huo kufanya usafi.
Ludigija amesema kutokana na zoezi la ufanyaji usafi kuonekana kuwa halikutiliwa mkazo hivyo ni vyema wananchi wakaendelea kufanya usafi wa kila Jumamosi ya Mwisho wa mwezi ili kujihadhari na magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na uchafu.
Amewakumbusha wananchi kuwa usafi ni wa kila mmoja hivyo wahakikishe kila mmoja kwa nafasi yake katika maeneo yanayomzunguka anafanya usafi na siyo kusubiri mpaka asukumwe na watu wa mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uhifadhi Mazingira na Udhibiti taka ngumu Manispaa ya Ilala Abdon Mapunda, amesema suala la usafi ni la kila mmoja hivyo amewasisitiza wananchi kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao kwani itawasaidia kuweka mazingira yao katika hali ya usafi.
Mapunda amesema kurudishwa kwa zoezi hilo la ufanyaji wa usafi kwa kila jumamosi litasaidia kuleta hamasa kwa wananchi jambo litakalosaidia waepukane na magonjwa ya mlipuko ,homa ya matumbo ,kipindupindu na kuhara.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Green Waste Pro (LTD )Deusdedit Rutazaa amewakumbusha wananchi kuwa taka sio suala la kampuni hiyo ya usafi pekee bali wahakikishe wanazihifadhi katika mifuko lakini pia walipe tozo za taka kwa wakati.
Hata hivyo Imeelezwa kuwa licha ya Manispaa ya Ilala kuzindua kampeni za ufanyaji wa usafi hii leo bado wananchi wataendelea kuhamasishwa kuzingatia ufanyaji wa usafi kwa kila Jumamosi ili kuifanya manispaa hiyo kuwa ya mfano wa kuigwa.






Post a Comment