SAKATA LA KUPANDA BEI YA CEMENT , RC KUNENGE ATEMBELEA KIWANDA ,MADUKA AT...
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge ameelekeza Maduka yote yanayouza Saruji kwenye Mkoa huo kuhakikisha wanauza kwa bei elekezi isiyozidi Tsh 15,000 na kumuelekeza Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa kuanza msako wa kuwakamata wote watakaokiuka agizo hilo.
RC Kunenge ametoa agizo hilo wakati wa ziara kwenye viwanda vinavyozalisha saruji na Maduka yanayouza saruji mkoani humo ambapo ameshangazwa kuona uzalishaji wa saruji kwenye viwanda ukiendelea Kama kawaida na kuuza kwa bei ya Tsh 12,500 lakini wauzaji wanauza kwa Bei ya Tsh 17,000 ambapo walipoulizwa kwanini wanauza kwa Bei hiyo wameeleza kuwa wanauziwa kwa Bei ya Tsh 14,500 kutoka Mawakala jambo ambalo amelieleza kuwa ni hujuma.
Kutokana na hilo RC Kunenge ametoa maelekezo kwa Wizara ya Viwanda na biashara na Afisa biashara wa Mkoa huo kupitia upya utaratibu wa uzalishaji na uuzaji wa saruji kuanzia ngazi ya kiwandani Hadi kwa mtumiaji wa mwisho ili kudhibiti upandaji holela wa bei.
Aidha RC Kunenge amesema tayari ameandaa kikosi kazi kitakachopita kwenye Maduka jijini humo na kuwakamata wote watakaouza saruji kwa Bei tofauti na ile iliyoelekezwa.
"Katika Mkoa huu chini ya Rais Dkt. John Magufuli hatuwezi kukubali upuuzi wa aina hii, hatukubali hujuma hii na hatukubali uroho na ulafi wa watu wachache wanaoumiza wananchi kwa maslahi yao binafsi, kuanzia wakati huu saruji kwenye Mkoa huu isiuzwe zaidi ya Tsh 15,000" Alisema RC Kunenge
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa amesema jeshi hilo limejipanga ipasavyo kuhakikisha wanafuatilia maeneo yote ya jiji hilo na kuwawajibisha wale wote watakaokiuka maelekezo hayo.
Post a Comment