Ads

NLD WAKUTANA KUMJADILI MWENYEKITI ALIYEMPIGIA DEBE MAALIM SEIF ZANZIBAR.

 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Upinzani nchini Tanzania National League for Democracy (NLD) Bw. Tozy Matwanga akizungumza na Waandishi wa habari Oktoba 17, 2020 Jijini Dar es Salaam.
....................
 Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Chama Cha Upinzani nchini Tanzania National League for Democracy (NLD) kimepinga kauli ya Makamo Mwenyekiti upande wa Zanzibar Bw. Hamadi Hemedi ambaye aliyedai kuwa watamuunga mkono mgombea wa urais wa Chama cha ACT- Wazalendo Maalim Seif Sharifu Hamadi.

Chama hicho kimeeleza kuwa msimamo wao watampigia kura mgombea wao Mfalme Hamisi Hassan katika nafasi ya urais Zanzbar katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Chama Cha NLD Tanzania Bara Tozy Matwanga, amesema kuwa leo Oktoba 18 mwaka huu, kamati kuu  watakaa kikao kwa ajili ya kumpa nafasi Bw. Hemedi aweze kujieleza kwa sababu gani ametangaza kumuunga mkono maalim seif bila kuwa na makubaliano na uongozi wa chama.

Bw. Matwanga amesema kuwa chama cha NLD hawana mpango wa kushirikiana  na vyama vyengine vya upinzani  kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 kwa sababu hawaoni faida zaidi ya kuwanufaisha baadhi ya vyama.

Katika hatua nyengine amebainisha kwa sasa Mwenyekiti wa Chama cha NLD ni Taifa Bw. Mfalme Hamisi Hassan na sio Bw. Oscar Makaidi kama ilivyokuwa inafahamika na watu wengine.

Bw. Matwanga amewataka watanzania kuwa na busara katika kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa salama na amani, kwani kuna baadhi ya wagombea wamekuwa wakitoa lugha za kuwachonganisha jambo ambalo sio rafiki.

“Tunawaomba watanzania kujiepusha na wanasiasa wanaotumia lugha za uchochozi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu ” amesema Bw. Matwanga.

Bw. Matwanga amempongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli baada kufuraishwa na utendaji kazi wake  ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara.

‘’Rais amefanya mambo mengi mazuri katika kipindi  cha miaka mitano ya uongozi wake” amesema Bw. Matwanga.

Mwenyekiti wa Idara ya vijana Taifa Chama cha NLD  Othiniel Mizizi, amesema kuwa wamejipanga kikamilifu kushiriki uchaguzi mkuu pamoja na kuendelea kuomba kuwe na amani katika uchaguzi huo.

No comments