TPDC YABAINI UWEPO WA VIASHIRIA VYA MAFUTA BONDE LA MTO MANONGA
Na Mwandishi wetu Shinyanga.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi wa utafutaji wa mafuta katika bonde la mto Manonga baada ya utafiti wa awali kubaini uwepo wa miamba yenye viashiria vya mafuta katika bonde la mto huo.
Mradi huo ujalikanao kama EYASI –WEMBELE unatatekelezwa katika Mikoa ambayo mto huo unapitia ikiwemo bonde la Ziwa EYASI na bonde la mto Manonga unaopatikana katika Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Singida na Manyara.
Akitambulisha Mradi huo kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga jana Mtaalam Mshauri wa Mradi huo Dkt. Allan Mzengi kutoka TPDC alisema Mradi huo unaanza na hatua ya awali ya kuangalia athari za kimazingira katika Wilaya Kishapu Mkoani Shinyanga hatua itakayoshirikisha wadau kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kata.
Dr. Mzengi aliuambia uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa pamoja na kuangazia suala la kimazingira hatua ya pili ya mradi itakuwa ni ujenzi wa Mkuza katika eneo ambao mradi huo utatekelezwa na baadae kuweka vilipuzi vitakavyosaidia kubaini maeneo ya ujenzi wa visima vya majaribio ya utafutaji mafuta katika eneo la mradi.
Aidha Mjilojia Kutoka TPDC Bw. Gaston Canuty aliuambia uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa tayari TBDC imeishachimba visima vifupi katika eneo la mradi kubaini miamba yenye uwezekano wa kuifadhi mafuta na sasa mradi huo unakusudia kwenda mbali zaidi kuangalia mafuta yako wapi chini ya Ardhi baada ya kubaini miamba hiyo katika eneo la Kishapu.
Ili kufanikisha zoezi hili Bw. Gaston aliongeza kuwa utafiti utatumia njia ya jiofizikia ambapo watajenga mikuza ambayo itawekwa vilipuzi laini ambavyo vitakapolipuliwa vitawawezesha kupata data chini ya ardhi itakayowawezesha kutambua mahali penye uwezekano wa mafuta.
Bi. Loveness Njogela ambaye pia ni Mjiolojia alisema utafiti wa Mafuta katika eneo la Mradi ulianza kwa tumia ndege ya utafiti ambayo iliwawezesha kuona maeneo yenye miamba yenye tabaka gumu na ile ya tabaka laini na kwa kanuni za kijiolojioa maeneo yale ambayo yana mkandamizo mkubwa wa miamba tabaka ndiyo yatakayofanyiwa jaribio la utafutaji mafuta.
Bi. Njogela aliongeza kuwa pamoja na baadhi ya maeneo kuwa na miamba yenye mgandamizo mkubwa inayotumika kama sampuli mafuta yana tabia kuama katika eneo la miamba hiyo na kutafuta mtego mahali pengine ndio maana wataweka vilipuzi laini vitakavyowezesha kutambua ni wapi kuna uwezekano wa kuwa na mtego wenye mafuta.
Wakati huo Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela alihaidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalam hao kwa lengo la kufanikisha utafiti huo ambao utafanyika katika kata za Mwamalasa, Gana na Mwamashele Wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga.
Post a Comment