Ads

Chuo Kikuu cha Mzumbe chawahimiza wanafunzi kuchangamkia fursa za kozi mwaka wa masomo 2020/21

Chuo Kikuu cha Mzumbe kimewahimiza wanafunzi waliohitimu kidato cha sita, ngazi ya cheti na astashada kuchangamkia fursa za kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho ikiwemo za utawala, tehama, biashara, uchumi na ujasiriamali ili wapate elimu bora pamoja na kuendana na soko la ajira.


Hayo yamesemwa na Makamu MKuu wa chuo hicho Profesa Lugano Kusiluka katika Maonyesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofikia kilele Septemba 5 mwaka huu katika Viwanja vya Mnazi Mmoja,Dar es Salaam.

Alisema kuwa sababu ya kuwahimiza wanafunzi kujiunga na kozi hizo ni kutokana na ubobeaji katika kuzifundisha hivyo amewataka kuchangamkia fursa hiyo.

" Watu waelewe mahali popote duniani  hauwezi kuendesha uchumi wa nchi bila ya kuwa na watalaamu wa fedha, sheria, biashara na wajasiriamali hivyo mtambue taaluma hizi zina umuhimu," alisema Profesa Kusiluka.

Alisisitiza kuwa chuo kinaendelea na maboresho ya miundo mbinu  kwenye matawi yote ikiwemo ujenzi wa bweni litakalochukua wanafunzi 900 katika Tawi la Mbeya.

Alifafanua kuwa katika mwaka wa masomo wa 2020/21  chuo hicho kupitia tawi la Upanga ambalo kwa muda mrefu linatoa shahada ya uzamili litatoa shahada ya kwanza.

Pia alisema Tawi la Dar es Salaam linajenga madarasa mapya eneo la Tegeta na kwamba wanafunzi wanakaribishwa kujisajili ili wasome masomo yatakayofundishwa.

Katibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo alitoa wito kwa vyuo Vikuu na taasisi kujikita kwenye tafiti za kuimarisha na kujenga uchumi wa viwanda.

Alisema hadi sasa serikali imekwishatoa Sh Trilioni 1.03 kugharamikia elimu ya msingi hali iliyochangia wanafunzi kuongezeka  kutoka mil 8.3 mwaka 2015 kufikia 10.9 mwaka huu.

Dkt Akwilapo alisema kuwa idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne imeongezeka kutoka mil 1.6 mwaka 2015 had I mil 2.2 mwaka Jana huku kidato cha sita wakiwa 153,000.

Mwenyekiti wa TCU Profesa Mayunga Nkunya, alisema Tume hiyo inaendelea kushirikiana na vyuo vikuu kwa kuvishauri kuandaa mitaala inayoendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

Profesa Nkunya  aliongeza kuwa TCU imeimarisha mifumo yake ya utoaji elimu kwa umma ili kuwafikia wadau wengi ikiwemo kudahili kampuni 14 zinazohusika na kudahili wa wanafunzi.

Katibu Mtendaji Mkuu wa tume hiyo Profesa Charles Kihampa alisema Maonyesho hayo yameshirikisha taasisi 67 huku kati ya hizo 58 zinatoa elimu ya Juu.

No comments