Ads

WIZARA YA KILIMO YAPONGEZWA KWA KUFUTA VYAMA VYA USHIRIKA 2,539

....................
Wizara ya Kilimo imepongezwa kwa uamuzi wa kuvifuta vyama vya ushirika 2,539 ambavyo vilikuwa na utendaji mbovu uliosababisha kero kwa wanaushirika nchini.

Pongezi hizo zimetolewa leo (03.08.2020) na Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu( Uwekezaji ) Angellah Kairuki wakati alipohutubia wananchi wa Simiyu kwenye maonesho ya Nanenane ikiwa ni siku maalum ya kuhamasisha ushirika.
Amesema hatua hiyo ya wizara itawezesha wanaushirika ambapo ni wakulima, wavuvi na wafugaji kunufaika na kazi zao ndani ya ushirika .
“ Ninawapongeza sana Wizara kwa hatua mliyochukua ya kuvifuta vyama vya ushirika 2,539 kwa sababu ya kutofanya kazi iliyokusudiwa.” alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki alisema katika kipindi cha 2018/2019 jumla ya viwanda 75 vimeanzishwa na vyama vya ushirika vinavyochata alizeti, chikichi,kutengeneza samani za majumbani,kuchakata pamba na mazao ya nafaka pamoja na usindikaji wa maziwa.
“ Viwanda vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka viwanda 133 mwaka 2018 hadi kufikia viwanda 208 mwaka 2019” alisema Waziri Kairuki.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (EGA) kuangalia namna bora ya kuweka mfumo shirikishi wa TEHAMA utakaoweza kuongeza uwazi katika usimamizi wa vyama vya ushirika hususan AMCOS.
Naye Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema wizara yake itaendelea kuhakikisha wakulima, wavuvi na wafugaji nchini wananjiunga na vyama vya ushirika ambavyo vitawasaidia kupata nguvu ya kuweza kupata mitaji,masoko,pembejeo na huduma za ugani ili wakuze uzalishaji.

Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa yameingia siku ya tatu leo ambapo wananchi na wakulima toka mikoa ya Mara,Simiyu na Shinyanga wanaendelea kupata elimu kwenye mabanda na vipando vilivyoandaliwa.
Kauli mbiu ya Nanenane mwaka huu inasema “ Kwa Maendeleo ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020”  

No comments