BOMBARDIER KUTUA SONGEA SEPTEMBA
Serikali imesema ndege aina ya Bombardier Q400 itaanza safari zake za kuruka na kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Songea ifikapo mwezi Septemba mwaka huu ili kufungua fursa za kiuchumi na kijamii.
Amezungumza hayo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akiwa mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya kukagua hali ya miundombinu ya barabara, madaraja na kiwanja cha ndege ambapo ameridhishwa na hatua zilizofikiwa za ukarabati wa kiwanja hicho ikiwemo unoreshaji wa barabara ya kutua na kuruka yenye urefu wa mita 1740, maegesho ya ndege na taa za kuongozea ndege.
"Hadi sasa hatua zilizofikiwa ni nzuri na kufikia mwisho wa mwezi huu wa nane mkandarasi atakuwa amekamilisha kujenga mita 1200 za barabara ya kuruka na kutua ndege ambayo itaweza kuruhusu ndege kubwa aina ya Bombardier kuanza kutua", amesema Waziri Kamwelwe.
Waziri Kamwelwe amesema kuwa ukarabati na uboreshaji wa kiwanja hicho unagharamiwa na fedha za ndani kwa kiasi cha shilingi bilioni 37 na unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2020.
Aidha, ameongeza kuwa kukamilika kwa kiwanja hicho kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo katika ukanda huo ambao awali ulikuwa na changamoto kubwa ya usafiri wa anga.
"Ujio wa ndege hizi utapunguza gharama za usafiri wa ndege ambapo awali gharama ya ndege ilikuwa fedha za kitanzania zaidi ya shilingi laki tano kwa safari moja na hii kupelekea watu wachache kumudu gharama hizo", amesisitiza Waziri Kamwelwe.
Waziri Kamwelwe ameeleza azma ya Serikali ni kuendelea na uboreshaji na ukarabati wa viwanja vingine 10 hapa nchini kwa lengo la kuinua na kukuza uchumi wa Taifa.
Awali akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Ruvuma Mhandisi Lazeck Alinanuswe, amemueleza Waziri huyo kuwa mpaka sasa mkandarasi amefikia asilimia 60 ya kazi ya ujenzi wa tabaka jipya la lami katika uwanja huo.
Mhandisi Alinanuswe, amefafanua kuwa uboreshaji na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Songea unatekelezwa na kampuni ya CHICO na kusimamiwa na kampuni ya Atkins J/V Advance Engineering kwa muda wa miezi 20.
Akizungumza kwa naiba ya wananchi wa Wilaya ya Songea Mjini, Bi. Sakina Hassan, ameeleza kufurahishwa kwake na ujio wa safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), ambazo zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria wengi pamoja na kupunguza muda na gharama za usafiri.
Waziri Kamwelwe yupo mkoani Ruvuma kwa muda wa siku mbili kwa ajili ya ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege.
Post a Comment