Ads

BASHUNGWA KUPITIA NANENE AMEWATAKA WAKULIMA KUZALISHA MAZAO YA KIPAUMBELE NA KIMUKAKATI


Na Eliud Rwechungura – 
Wizara ya Viwanda na Biashara Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa amewataka wakulima Kupitia maonesho ya kitaifa ya Wakulima "NaneNane" kuendelea kuzalisha kwa wingi mazao ya kipaumbele na ya kimukakati ili kuokoa mabilioni ya fedha kwenda nchi za nje na badala yake kutumiwa hapa hapa nchini. Bashungwa ameyasema hayo August 05, 2020 alipokuwa mgeni rasmi kwenye Maonesho ya kitaifa ya Wakulima "NaneNane" yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu katika viwanja vya Nyakabindi yenye kauli mbiu inayosema ‘‘Kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua viongozi bora 2020’’. ‘‘Kupitia maonesho haya, naomba kuwatia moyo na kuendelea kuzalisha kwa wingi hususani mazao ya kipaumbele na ya kimukakati kama vile korosho, pamba, kahawa, chai, tumbaku na michikichi, mazao ya bustani, vyakula vya ngano, mafuta ya kula, sukari na mbegu za mahindi ili kuokoa mabilioni ya fedha kwenda nchi za nje na badala yake kutumiwa hapa hapa nchini’’ amesema Bashungwa Bashungwa amewapongeza washiriki wote walioshiriki maonesho hayo kwa kuonesha teknolojia mbalimbali ambazo zinawapa fursa watembeleaji kujifunza na kwenda kutumia utaalamu huo kuzalisha kutokana na teknolojia wanazoziona kwenye maonesho hayo ambazo kwa asilimia kubwa zinachangia ongezeko la viwanda ambapo Katika kipindi cha miaka mitano ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Sekta ya Viwanda imeendelea kukua ambapo hadi mwezi Aprili 2020 jumla ya viwanda vipya 8,477 vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini kati ya mwaka 2015 hadi 2019 na hivyo kuwezesha ongezeko la ajira 482,601 viwandani. Viwanda hivyo vipya vinajumuisha viwanda 201 vikubwa, 460 vya kati, 3,406 vidogo; na 4,410 vidogo sana. Aidha, Bashungwa ametumia nafasi hiyo kuelezea namna Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo zilivyojipanga kufungamanisha kilimo na viwanda na akatoa takwimu ya vyakula vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi. ‘‘Ongezeko hilo la viwanda linaenda sambamba na tija kwenye kilimo, mifugo na uvuvi ambapo ndio vyanzo vikubwa vya malighafi katika kuendesha viwanda hivyo. Na katika kufanikisha hili, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo zinafanya kazi bega kwa bega kuhakikisha tunafungamanisha kilimo na viwanda, Takwimu za import ya vyakula inaonesha mwaka 2014-2019 import bill ilikuwa takribani trillion 1.3 kwa mwaka. Kwa miaka hiyo sita import bill ilikuwa trillion 7.738. Katika hili, ngano ni 53.3% ya import, mafuta ya kula 22.6%, sukari 16.2% na mbegu za mahindi 2.8%. Items nyingine zote ni chini ya 1%. Sukari tumepiga hatua kubwa lakini nayo ni kwa sababu uliliwekea mkazo chini ya uongozi wa Rais.’’ Sambamba na hayo Bashungwa ameagiza Taasisi ya SIDO kukaa na Mkoa wa Simiyu kuangalia model ya fedha zinazotenga kwa ajili ya mikopo kwenye halmashauri, kubuni miradi ambayo itakuwa endelevu na kusaidia makundi mbalimbali yakiwemo, wakina mama, vijana na walemavu. Aidha, SIDO kwa niaba ya Wizara wafanye ufuatiliaji kwa kila Halmashauri kutenga maeneo na kuleta taarifa ya Halmashauri zilizokwisha tenga maeneo na zile ambazo bado. Bashungwa amemalizia kwa kusisitiza kuwa Wizara itaimarisha taasisi zake ili ziweze kukidhi na kuhimili mahitaji ya maendeleo na ujenzi wa viwanda nchini. Wizara itajikita kuimarisha Taasisi za Utafiti na Maendeleo ya Teknolojia yaani TIRDO, TEMDO na CAMARTEC kwa kufanya tathmnini ya kitaalam, kupitia upya na kwa kina majukumu na miundo ya kisheria ya taasisi hizo.

No comments