MANISPAA MOROGORO YAJA NA SULUHISHO LA KUPUNGUZA USUMBUFU KWA WANANCHI KUFUATA DAWA MADUKA BINAFSI
Ujenzi wa Duka la Dawa Kituo cha Afya Sabasaba ukiendelea. |
HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro, imeaamua kutekeleza kwa vitendo agizo la TAMISEMI la kutaka kila Halmashauri kuwa na Duka la dawa.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro ,Dr Ikaji Rashid, amesema mara baada ya kukamilika kwa mradi huo ,utasaidia kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wakazi wote wa Kata 29 za Manispaa ya Morogoro .
Dr. Ikaji, amesema , faida nyengine ya mradi utasaidia kupunguza usumbufu wa wateja kufuata dawa maduka binafsi na kuongeza mapato ya kituo na Halmashauri kwa ujumla.
Aidha, amesema kuwa kwa mujibu wa tathmini ya BoQ , mradi huo utakapokamilika unategemea kugharimu kiasi cha Tshs Milioni 24,572,054/=
“Tumetekeleza agizo la TAMISEMI la kutaka kila Halmashauri kuwa na Duka la dawa kwa kutumia mapato ya ndani ya Kituo hiki cha afya , lakini pia duka hili la dawa litakuwa mkombozi kwa wananchi wetu wa Manispaa kwa ajili ya kupata dawa kwa bei halisi ya Serikali na kuwapunguzia umbali mrefu na usumbufu wateja wetu kufuata dawa kwenye maduka binafsi, mpaka sasa mradi huu umetekelezwa kwa asilimia 85% na ujenzi upo kwenye hatua ya mwisho ya umaliziaji ambapo kazi zilizo bakia ni upigaji wa rangi, kuunganisha umeme, mfumo wa Elektroniki na samani” Amesema Dr. Ikaji.
Hata hivyo, amesema kutokana na Ugonjwa wa CORONA mapato ya kituo kwa sasa yameshuka pamoja na kituo hicho kuelemewa na gharama kubwa za ukarabati na ununuzi wa vifaa vya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA kwa watumishi .
“”Tumebakiza sehemu ndogo ya ujenzi, tunaomba msaada wa Mbunge wetu wa Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood na Mkurugenzi wa Manispaa na wadau mbalimbali watusaidie ili kukamilisha mradi huu kwa kazi ambazo zitagharimu jumla ya shilingi Milioni 16,265,100/=” Ameongeza Dr. Ikaji.
Amesema miongoni mwa vitu vinavyohitajika katika kukamilisha ujenzi uliobakia ni pamoja na kuweka mfumo wa Elektroniki wenye thamani ya shilingi, 4,499,000/=, Samani (Shelf na kabati za Aluminiamu Tshs 9,021,100/=, Kiyoyozi (AC) Tshs 1,800,000/= pamoja na Gharama za kuunganisha umeme katika duka Tshs 445,000/=.
Katika hatua nyengine, amesema amesema Kituo kimefanya ukarabati mkubwa wa vyoo na mfumo wa maji taka ndani ya Kituo na kuunganisha mfumo huo kwenye mtandao wa maji taka wa MORUWASA ambapo mpaka sasa tayari Kituo kimeunganishwa kwenye mtandao.
Amesema Kituo kimeanza ukarabati wa Kitengo cha kinywa na meno ambapo katika Mnaispaa huduma hii hutolewa katika Kituo hicho na ukarabati huo unalenga kuboresha huduma hizo na kukifanya kitengo hicho kuwa cha mfano katika Manispaa ya Morogoro .
Amesema Vifaa vya kisasa kwa ajili ya kitengo hicho vimeshaagizwa kupitia MSD huku ukarabati wa kitengo hicho pamoja na ununuzi wa vifaa utagharimu Tshs milioni 72,000,000/= ambapo chanzo cha fedha hizo za ukarabati zimetoka katika mfuko wa pamoja (Basket Fund).
Mwisho, amesetoa shukrani za kipekee kwa niaba ya Watumishi wa Kituo cha Afya Sabasaba, Mhe. Diwani wa Kata ya Sabasaba na kamati ya usimamizi kwa Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood kwa kuwapatia gari pamoja nafedha za kuunganisha Umeme kwenye duka la dawa ambapo amesema matukio hayo yatabakia kuwa kumbukumbu kubwa isiyofutika kwa Kituo cha afya pamoja na Manispaa kwa ujumla.
Post a Comment