NEEMA ZANZIBAR, SMZ YAPATA GAWIO LA BILIONI 25
Na Iddi Haji, Maelezo, Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imepata faida zaidi ya shilingi bilioni 25 ikiwa ni malipo ya huduma
za matumizi ya mkonga wa taifa, Serikali mtandao Visiwani Zanzibar
Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa
Mkonga wa Mawasiliano Zanzibar, Mhandisi Shukuru Awadhi Suleiman amesema
kwamba fedha hizo zimelipwa kutoka katika makapuni ambayo yanatumia
huduma zao.
“Tumepata fedha hizo ambazo kutoka
Kampuni ya simu ya ZANTEL ikiwa ni malipo kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka
2024” Alisema Mkurugenzi huyo.
Alisema kwamba Serikali mtandao
imekuwa na faida kubwa kwa wananchi ambapo sasa huduma za afya, kodi na
elimu zimekuwa zikitolewa kwa urahisi na ufanisi mkubwa.
Amesema katika sekta ya afya,
kumekuwa na mafanikio makubwa katika huduma, vituo vya afya 24 Unguja na
Pemba vimeunganishwa katia mfumo wa Serikali mtandao.
“Leo hii mgonjwa anaweza kufanyiwa
vipimo kama vya X-ray katika hospitali ya Kivunge Mkoa Kaskazini Unguja
na, vipimo vile vitasomwa Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja bila ya mgonjwa
au daktari kulazimika kusafiri” Alisema Mkurugenzi Mhandisi Shukuru.
Mkuruhenzi huyo amesema kwa
kutumia huduma za Serikali Mtandao, huduma za vyeti vya kuzaliwa imekuwa
rahisi kwa sasa kwani wananchi wanapata vyeti vya kuzaliwa katika
Wilaya zao.
“Sasa hivi Wakala wa Usajili na
Matukio ya Kijamii Zanzibar wanatumia huduma hizi, watu wanapata vyeti
vyao vya kuzaliwa katika Wilaya zao, wanaomba huko na taarifa zao
zinatumwa Makao Makuu na kufanyiwa kazi” Alisema Mkurugenzi Shukuru.
Mbali ya sekta hizo, pia Kampuni
ya Uunganganishaji Maudhui ya ZMUX inatumia mkonga wa taifa katika
kurusha matangazo ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Akizungumzia sekta ya kodi,
Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kwamba Bodi ya Mapato Zanzibar ni moja
ya watumiaji wakubwa wa huduma za Serikali mtandao ambapo sasa huduma
za kodi zimeunganishwa katika mtandao mmoja.
Amesema tayari wamepokea maombi ya makampuni ya simu, TTCL, na kampuni ya Comnet kutaka kutumia huduma za mkonga wa taifa.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya
Mawasiliano, Dkt Mzee Suleiman amesema kumekuwa na mafanikio katika
matumizi ya TEHAMA hasa baada ya kukamilika kwa mkonga wa taifa.
Dkt Mzee amesema mwaka 2011, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohamed Shein
alitoa agizo la kuhakikisha Zanzibar inaongeza kasi ya matumizi ya
TEHAMA katika shughuli mbalimbali.
Mkurugenzi huyo amesema kuna vituo
10 vya kuwafundisha wananchi matumizi ya teknolojia ya habari na
mawasiliano, ambapo mafunzo hayo yanatolewa bure kwa wananchi.
Post a Comment