Ads

CUF YAMUOMBA JPM KUINGILIA KATI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MTAA.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Chama cha Wananchi CUF kimemuomba Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuingilia kati zoezi la kuwachagua wagombea wa uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umeonekana kwenda kinyume na taratibu katokana na wagombea wa upinzani kuondolewa kwa kile kinachodaiwa hawana vigezo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kuwa wasimamizi wa uchaguzi wamekuwa hawafati kanuni na taratibu za uchaguzi, kwani wagombea wa CUF wameondolewa bila sababu ya msingi.

Amesema kuwa kutokana na kile kinachoendelea kuna uwezekano katika uchaguzi huu kuna mpango wa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupita bila kupigwa kutokana kile  wagombea wa upinzani kuondolewa.

"Kama wagombea wa serikali za mitaa wakipita bila kupigwa...basi katika nafasi ya udiwami, ubunge itakuwa hivyo hivyo" amesema  Profesa Lipumba.

Amesema kuwa ni busara kuwapa fursa wananchi kuwachagua viongozi wanaowataka kuliko kuwachagulia viongozi.

Amesema kuwa uchaguzi huu upo chini ya Ofisi ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), hivyo ni vyema kuingilia kati ili kuleta usawa katika demokrasia.

Profesa Lipumba amebainisha kuwa ameandaa mapendekezo ambayo anatarajia kumpelekea Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili aweze kuyafanyika kazi.

Uchaguzi wa serikali za mtaa unatarajia kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

No comments