WAZIRI HASUNGA AVIAGIZA VYAMA VYA USHIRIKA KUSHIRIKI KATIKA UNUNUZI WA MBOLEA KWA PAMOJA (BPS)
Kutokana
na kuwepo kwa mfumo wa ununzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) serikali
imeviagiza Vyama vya ushirika vya msingi (AMCOs) na vyama vikuu (FCU)
kuanza kushiriki kwenye ununzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) ili
kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa bei nafuu na kwa wakati.
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa agizo hilo wakati akizungumza
kwenye maadhimisho ya siku ya mbolea Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika
leo tarehe 13 Octoba 2019 katika viwanja vya shule ya msingi Kashaulili
Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Amesema
kuwa ili kuongeza matumizi ya mbolea nchini, Wizara ya kilimo kupitia
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeweka mikakati
mbalimbali ya kuhakikisha mbolea inapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu
ikiwemo mfumo wa unuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS).
Pia,
imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoa elimu
kwa njia tofauti kwa lengo la kuongeza uelewa wa umuhimu na kuongeza
matumizi ya mbolea nchini hivyo ili tija na uzalishaji viongezeke vyama
vya ushirika havina budi kushiriki kwenye ununuzi wa mbolea ili
kuwarahisishia wanachama wao ambao ni wakulima kupata mbolea kwa wakati
na kwa bei nafuu.
Mhe
Hasunga ametoa mwito kwa wafanyabiashara wa mbolea kuuza mbolea kwa bei
elekezi iliyopangwa na serikali na wazingatia bei hizo kwa mbolea za
kupandia (DAP) na kukuzia (UREA) ambazo zinaingizwa nchini kwa mfumo wa
Uingizaji wa Mbolea kwa Pamoja yaani Bulk Procurement System BPS.
“Kama mnavyofahamu, Serikali imeendelea kuratibu utoaji wa mikopo yenye riba nafuu kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (Tanzania Agriculture Development Bank-TADB), Benki ya Uwekezaji (Tanzania Investment Bank TIB) na
Mfuko wa Pembejeo wa Taifa. Hivyo, nitoe wito kwa wakulima wote wa Mkoa
wa Katavi na Mikoa mingine kujiunga katika ushirika ili kuweze kutumia
fursa zinazotolewa na taasisi hizi ili kujiletea maendeleo” Alikaririwa
Mhe Hasunga
Waziri
Hasunga amesema kuwa ili kuwa na matumizi sahihi ya mbolea, ufahamu juu
afya ya udongo ni muhimu; hivyo, ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
Tanzania (TARI) kutoa taarifa ya afya ya udongo kwa wakulima na wadau
wengine ili matumizi ya mbolea yaendane na mahitaji ya zao na udongo
husika.
Niwakumbusha
wafanyabiashara wakubwa kuwa mbolea zinahitajika zaidi mikoani; hivyo
ni wakati muafaka wa kuanza kusambaza mbolea mikoani haraka
iwezekanavyo. Pia ni wakati sahihi wa kufungua matawi ya mauzo na
maghala mikoani badala ya mbolea nyingi kurundikana kwenye maghala
yaliyoko Dar es salaam ambako mahitaji yake ni madogo.
Ameongeza
kwa kusema kuwa ili mbolea iweze kuwafikia wakulima kwa wakati,
amelitaka shirika la reli Tanzania (TRC) kutoa kipaumbele katika
usafirishaji wa mbolea kwa mikoa ya Tabora, kigoma na Katavi huku
akiitaka Mamlaka ya udhibiti wa mbolea (TFRA) kuhakikisha inasimamia
ubora wa mbolea kuanzia bandarini inapoingia hadi kwa muuzaji
anayemuuzia mkulima.
Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni ‘matumizi sahihi ya mbolea kwa uhakika wa chakula na uchumi wa viwanda’. Ambapo lengo
la maadhimisho ya siku ya mbolea duniani nchini Tanzania ni kupata wigo
mpana zaidi kwa Wadau kuelezea masuala mbalimbali katika tasnia ya
mbolea.
Masuala
hayo ni pamoja na mafaniko ya tasnia ya mbolea nchini, kuwahabarisha
wadau wa mbolea hususani wakulima na wafanyabiashara wa mbolea mifumo
mbalimbali ya upatikanaji na usambazaji wa mbolea; pia kutoa elimu
kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia tasnia ya mbolea.
Siku
ya mbolea duniani ilianza kuadhimishwa kwa mara ya kwanza tarehe 13
Oktoba, 2016 huko nchini Uingereza. Siku hii ilianzishwa mahsusi kwa
lengo la kuhamasisha Wadau wa tasnia ya mbolea duniani kote kutambua
jukumu kubwa walilonalo la kuhakikisha kuwa wakulima wanatumia mbolea
bora na sahihi ili kuleta mapinduzi ya kijani kwa uhakika wa chakula.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe Juma Homera amesema kuwa tayari serikali
imetangaza bei elekezi ya mbolea hivyo wafanyabiashara watakaokiuka na
kuanza kuuza kwa bei zaidi ya hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Amesema
kuwa serikali inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli
imedhamiria kuwanufaisha wakulima kwenye sekta ya kilimo hivyo kukiuka
maelekezo ya serikali kwa wafanyabiashara wa mbolea hawana tofauti na
wahujumu uchumi.
Akizungumzia
kuhusu uzalishaji wa mazao ya chakula amesema kuwa mkoa wa Katavi kwa
kushirikiana na Wizara ya Kilimo utahamasisha wakulima kulima mazao
mengi kwa tija ili kuongeza uzalishaji utakaoimarisha usalama wa chakula
nchini.
Kwa
upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA)
Dkt Steven Ngailo amesema kuwa mbolea kwa ajili ya kukuzia na kupandia
tayari imewasili nchini hivyo wakulima wana fursa mahususi kabisa ya
kujitokeza na kuendeleza sekta ya kilimo katika kuongeza uzalishaji wa
chakula kwa ajili ya biashara.
Ameitaja kuwa siku ya mbolea Duniani ni kumbukizi ya maadhimisho ya uvumbuzi wa mbolea aina ya Amonia uliofanywa
na Bwana Fritz Haber mwaka 1908. Uvumbuzi huo ulichochea mapinduzi ya
kijani katika karne ya 20 yaliyowezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa
mazao kutokana na matumizi ya mbolea yaliyosaidia kupunguza kwa kiasi
kikubwa janga la njaa na kuleta uhakika wa chakula katika nchi nyingi
duniani.
Post a Comment