NAIBU WAZIRI MABULA AWATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA ZOEZI LA URASIMISHAJI.
Mwambawahabari
Na Munir Shemweta, WANMM ILEMELA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wananchi
kuchangamkia zoezi la urasimishaji linaloendelea nchini ili waweze kuwa na
umiliki halali wa ardhi yao watakayoweza kuitumia kujiletea maendeleo.
Dkt Mabula ambaye ni
Mbunge la Ilemela mkoani Mwanza alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki
alipozungumza na wananchi wa jimbo lake katika Mtaa wa Kabanganya kata ya
Bugogwa wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza akiwa katika ziara yake ya kukagua
utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika Kanda ya Ziwa.
Alisema, Rais wa
Jamhuri ya Muungano John Pombe Magufuli ameelekeza maeneo yote yaliyokuwa
katika ujenzi holela yarasimishwe kwa kupimwa ili wananchi wake wawe na umiliki
halali kwa kuwa walitumia nguvu nyingi wakati wa kuyaendeleza.
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kupimiwa pekee katika maeneo
yaliyorasimishwa hakutoshi na kushauri wananchi kuhakikisha wanapata hati za
umiliki ili waweze kuzitumia katika kujipatia mikopo na shughuli nyingine za
kimaendeleo.
‘’Wananchi walijenga
kwa nguvu zao, serikali haikuwa makini katika kupanga maeneo ili watu wakae
katika mpangilio mzuri hivyo Rais aliagiza wananchi warasimishiwe ili waweze kuwezeshwe kiuchumi na
kutumia ardhi yao na majengo kuendelea katika shughuli za uchumi na kuweka
dhamana na zoezi hili linafanyika kwa miaka kumi na kumalizika 2023’’ alisema
Dkt Mabula.
Akizungumzia shughuli
za maendeleo katika jimbo lake la Ilemela, Dkt Mabula alisema tangu achaguliwe
kuwa Mbunge wa jimbo hilo amefanya mambo
makubwa katika sekta ya elimu kwa kuwezesha ujenzi wa shule za msingi na
sekondari sambamba na kuongeza vyumba vya madarasa kwa baadhi ya shule hizo
tofauti na miaka ya nyuma.
Pamoja na mambo mengine,
Dkt Mabula aliwaambia wananchi wa mtaa wa Kabangaja kata ya Bugogwa mkoani
Mwanza kuwa, hivi sasa jitihada inafanyika kuondoa tatizo la maji katika mtaa wa
Kabangaja na mitaa mingine ya jimbo hilo ambapo tayari timu ya wataalamu iko
katika mtaa huo kuhakikisha inakamilisha uwekaji miundombu ya maji.
Baadhi ya wananchi wa
jimbo la Ilemela katika mtaa wa Kabangaja walimueleza Dkt Mabula kuwa
wanakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji katika maeneo yao ingawa mtaa wao ndiyo
chanzo cha maji kuelekea maeneo mengine.
Mkazi wa Kabangaja Aziz
Said alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa pamoja
na uwepo zoezi la upimaji shirikishi katika eneo hilo lakini hadi sasa bado hawajapatiwa
hati za umiliki wa maeneo yao jambo lililofafanuliwa na afisa Mipango Miji na
Ardhi kutoka Manispaa ya Ilemela William Magoha kuwa limesababishwa na baadhi
ya wananchi kushindwa kukamilisha fedha za upimaji.
Post a Comment