Serikali kupitia Sera ya Kilimo kupambana na mabadiliko ya hewa yawahimiza vijana kushiriki kwenye kilimo
Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kuipitia na kuifanyia maboresho Sera ya Kilimo ili iweze kuendana na mazingira ya sasa ikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi, changamoto za masoko ya uhakika ya mazao na pembejeo zenye ubora na matumizi ya teknolojia.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania, Nicholaus Mauye katika Fainali ya Tuzo za Kwanza za Shindano la kuwatafuta Vijana Mahiri wanaojihusisha na kilimo lililoandaliwa na Kampuni ya Transcend kwa Ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi pamoja na wadau wengine wa kilimo.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji iko katika mapitio ya sera hiyo kutokana na kutokidhi changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo katika mazingira ya sasa hasahasa mabadiliko ya tabia ya nchi.
" Wizara inachukua jitihada za kuboresha sekta ya kilimo imeanza kuipitia sera ya kilimo ili iendane na mazingira yaliyopo ukizingatia mabadiliko ya tabia ya nchi yana athari kubwa kwa wakulima wetu hivyo juhudi za dhati zinahitajika kupambana na hali hiyo," alisema Mauye.
Alibainisha kuwa Serikali katika kuboresha sekta hiyo imefanya mambo makubwa katika uboreshaji wa miundo mbinu zikiwemo barabara na madaraja na kwamba mkazo unatakiwa kuwekwa kwenye maeneo ya wazi kwa kufanya kilimo chenye tija.
Alisisitiza kuwa endapo Tanzania itaweka nguvu katika maeneo hayo itakuwa mzalishaji mkubwa wa chakula Afrika hasahasa kupata fursa kuuza mazao ya biashara katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Aliwahimiza vijana washiriki wa tuzo hizo waongeze ubunifu wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula cha kutoka cha ndani na kitakachouzwa kwa nchi wanachama wa SADC.
Aliishauri jamii kuondokana na dhana potofu kuwa kilimo ni cha wazee badala yake washiriki wakawe mabalozi kuhamasisha vijana wenzao wajiingize katika shughuli za uzalishaji mazao na ufugaji ili wajiongezee vipato, afya na kuingizia nchi fedha za kigeni.
Aliushukuru ubalozi wa nchi hiyo kwa kusaidia programu hiyo ya vijana huku aksisitiza Serikali inatekeleza Sera ya Viwanda kwa kujenga viwanda vidogovidogo lengo likiwa kuchakata mazao madogo madogo yanayozalishwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bonasi Siza alisema mchakato wa tuzo hizo ulianza mwezi Mei ambapo washiriki 300 walijitokeza kujisajili na kwamba vijana tisa tu waliofanikiwa kuvuka mchujo hadi kuingia fainali hiyo.
Alisema tuzo hizo zimebuniwa kutokana na asilimia 75 ya watanzania wanajihusisha na kilimo na kuwafanya vijana watambue umuhimu wa kilimo na kwamba washindi watapata fursa ya kukutana na wadau wa sekta hiyo.
Naye Jaji Levian Ngaiza alisema washiriki walioshinda wamepimwa kwa vigezo vya mradi kujali mazingira, ubunifu wa mradi, ubora wa mazao ya mradi, mradi una uendelevu pamoja na teknolojia inayotumika kwenye uzalishaji.
Balozi wa Uholanzi Nchini, Jerome Low aliwapongeza washiriki wote walioanza mwanzo hadi waliongia fainali na kusisitiza kuwa elimu ya kilimo chenye inahitajika kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao.
Katika shindano hilo katika Kipengele cha Kilimo cha mbogamboga na matunda nafasi ya kwanza ilichukuliwa Dickson Alex, ya pili Huruma Konga, ya tatu ilikwenda kwa Neema Masawe huku Kipengele cha Kilimo Cha Viazi Mviringo mshindi wa kwanza alikuwa Ebrania Mgeni, wa pili Clemence Mahenge huku ya tatu ikichukuliwa na Naomi Mwairasi.
Kipengele cha mwisho cha Ufugaji wa Kuku nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Kikundi cha Tusumuke kutoka Dodoma, ya pili ilichukuliwa na Adeline Malaki na ya tatu alipata Bwisungo Chakutema (Shinyanga).
Washindi wa shindano hilo walikabidhiwa vyeti, vikombe, fedha na ahadi ya kusaidiwa kupatiwa mafunzo kwenye uzalishaji, vitendea kazi na utafutiwaji wa masoko ya uhakika wa mazao wanayozalisha.
Post a Comment