Ads

Manispaa ya Iilala yataja siri ya mafanikio ya kuvuka malengo ya ukusanyaji kodi mwaka wa fedha 2018/19




Hussein Ndubikile, Mwambawahabari

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imetaja siri ya mafanikio yaliyoiwezesha kuvuka malengo ya ukusanyaji kodi ya Sh bilioni 57 ambapo katika mwaka wa fedha unaoishia June 2019 imekusanya Sh bilioni 58 sawa na asilimia 102 huku ikibainisha ushirikishwaji kati ya watendaji na wananchi umechangia mapato kuongezeka, uimarishaji wa ufuatiliaji mfumo wa kielektroniki pamoja na matokeo ya kodi wanayotozwa wananchi kuonekana inavyofanya kazi katika miradi ya maendeleo.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Mweka Hazina wa manispaa hiyo, Tulusubya Kamalamo katika Kikao cha kupitia Taarifa za Mwaka wa Fedha unaoishia mwezi Juni mwaka huu ambapo alisema siri kubwa ya mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano uliopo kati ya watendaji wa manispaa na madiwani pamoja na wananchi wanaona thamani ya kodi wanayolipa inavyotumika kwenye miradi hiyo ikiwemo ya ujenzi wa barabara, shule, vituo vya afya na Zahanati.

Alibainisha kuwa baada ya wananchi kuona matokeo ya kodi wanayolipa wamepata mwamko mkubwa wa kulipa kwa hiari bila kulazimishwa na kusababisha manispaa kuvuka malengo iliyojiwekea.

Alisisitiza kuwa ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za maendeleo ya miradi husika umechangia wananchi kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo kwenye kata zao hahasa ujenzi wa miradi huduma muhimu za kijamii.

Alifafanua kuwa ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutokana na Menejimenti ya manispaa kuweka mfumo madhubuti wa Kielektroniki kwenye kukusanya kodi katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kiwalani, Musa Kafana alisema siri ya mafanikio hayo ni matokeo ya kodi inayolipwa kuonekana katika kata 36 zilizopo ndani ya manispaa huku akibainisha katika kata yake barabara 14 zimejengwa kutokana na mapato yanayokusanywa kutoka kwa wananchi.

Kafana alisema hata Miradi Mikubwa ya Maendeleo (DMDP) inayotekelezwa ndani ya manispaa hiyo ni matokeo ya kodi ya wananchi inayokusanywa katika nyanja tofauti.

Naye Diwani wa Kata ya Mchafukoge, Mariamu Lulida alisema asilimia 28 ya miradi inatekelezwa katika kata yake na kwamba mafanikio ya utekelezwaju huo umechangiwa na ushirikishwaji kati ya watendaji, madiwani na wananchi.

Katika hatua nyingine, Meya wa Manispaa hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata wa Vingunguti, Omari Kumbilamoto amemwagiza Mganga mkuu wa manispaa pamoja na watu wa idara ya fedha kuhakikisha fedha za kununulia saruji zinapatikana ili ujenzi wa Hospitali ya Kivule uendele na kwamba wasivyofanya wote ataweka ndani.

No comments