Ads

Lions Club of Dar es Salaam Host chawahimiza wazazi wapeleke watoto wakapatiwe Chanjo ya Surua-Rubela



Hussein Ndubikile,
 Mwambawahabari
Wazazi nchini wameshauriwa kuondokana na dhana potofu kuwa Chanjo ya kukinga Magonjwa ya Surua na Rubela ina madhara kiafya kwa watoto badala yake wamehimizwa na kuhamasishwa kuwapeleka watoto wao wakapatiwe chanjo hiyo itakayoanza kutolewa bure kuanzia Septemba 26 hadi 30 mwaka huu nchi nzima katika vituo vya afya, zahanati na hospitali.

Ushauri huo umetolewa na Lion Aqeel Abbas Asharia kutoka Chama cha Lions Club of Dar es Salaam Host ambapo alisema wazazi hawatikiwi kujenga dhana potofu kuwa chanjo za magonjwa hayo zina madhara na kwamba wawapeleke watoto chini ya miaka mitano wakapewe chanjo ili waweze kuwakinga na magonjwa ya masikio, vidonda vya macho, Nimonia na utapiamlo.

Alibainisha kuwa chanjo hiyo ni bure hailipiwi na kwamba wazazi wanatakiwa kuhamasika kupeleka watoto wakakingwe na wasipatwe na magonjwa yanayosababishwa na Surua pamoja na Rubela.

" Chama chetu kinajishughulisha na utoaji huduma za afya na misaada mbalimbali kwa jamii  tunafanya kampeni ya kuhamasisha chanjo Rubela na Surua ili tuokoa maisha ya watoto waweze kukua vizuri kiafya na kiakili," alisema Lion Aqeelabbas.

Aliisisitiza kuwa chama hicho kinafanya jitihada mbalimbali za kuihamasisha jamii ikiwemo kuweka kambi za kutoa elimu na matibabu ya chanjo hiyo huku akisisitiza wanaunga mkono Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo hiyo inayotolewa bure nchi nzima.

Alifafanua kuwa chama hicho kitashiriki katika utoaji chanjo hiyo watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano katika Hospitali ya Apollo, Al Hilal na Rhemtulah zilizopo katikakati ya Jiji la Dar es Salaam.

Pia alisema mwezi Machi mwaka huu waliweka kambi katika Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni na kwamba walitoa huduma za meno, macho, sukari na presha huku akibainisha chama hicho kinajitolea wala hakifahidiki kwa huduma wanazozitoa bure.

Kwa upande wake Lion Mahmood Rajvani aliwasisitiza wazazi kutopuuzia chanjo hiyo kwani inatolewa kwa ajili kuwakinga watoto dhidi ya ulemavu unaosababaishwa na  Magonjwa ya Surua na Rubela.

Aliongeza kuwa mwezi Disemba mwaka huu wataweka kambi ya kupima na kutibu Magonjwa ya Presha, Macho na Meno kwenye Mikoa ya Lindi na Morogoro lengo likiwa kuisaidia jamii kupata huduma za afya bure.

No comments