Kanisa la Mennonite Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani lawapatia wakfu viongozi wake
Kanisa la Mennonite Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani limewapatia wakfu viongozi wake wapya na kuwataka kuendelea kuwajengea imani waumini pamoja na kuwaelekeza kutenda mambo mema ya kiroho.
Miongoni mwa viongozi waliopatiwa wakfu ni Katibu wa Dayosisi hiyo, Moses Ndege ambaye amechaguliwa kwa mara nyingine kuendelea kuongoza nafasi hiyo kwa muda wa miaka mitatu.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa dayosisi hiyo, Mchungaji Abner Mathube, Naibu Katibu, Justine Kussaga, Mtunza Hazina, Victor Gidion na Mchungaji Mwakilishi Baraza la Maaskofu Mchungaji Nelson Aketch pamoja na viongozi mbalimbali waliochaguliwa kuongoza nafasi zingine.
Akihutubia jijini Dar es Salaam katika Ibada ya kuwapatia wakfu viongozi hao Askofu wa Kanisa hilo wa dayosisi hiyo, Nelson Kisare alisema viongozi wote waliochaguliwa wanatakiwa kutimiza majukumu yao kwa kufuata misingi ya Yesu Kristu.
“ Tumewapatia wakfu tunaamini wamo mikononi mwa Mungu tuna mataumaini nao makubwa watatenda majukumu ipasavyo kwani wote waliochaguliwa kwa mfumo wa demokrasia unaotumiwa na kanisa,” alisema Askofu Kisare.
Alibainisha kuwa katika ulimwengu wa leo kuna manabii wanaohubiri utajiri huku akisisitiza kanisa hilo limejikita katika kuhubiri habari njema ya Yesu Kristu ili dunia ipate kuokoka.
Aliwahimiza wakristo kumpenda Mungu kwa kutenda matendo yanayompendeza na kwa kuishi maisha ya Yesu Kristu.
Askofu Kisare alisema kanisa hilo lilianzishwa mwaka 1934 na Wamisionari wa Wamarekani na wao ni sehemu ya makanisa ya Anabaptist ambayo hayabatizi watoto bali huwabatiza watu wazima.
Kwa upande wake Mchungaji wa kanisa hilo-Dayosisi ya Mashariki na Pwani Maira Migire alisema kuwa ifikapo mwaka 2034 kanisa hilo litatimiza miaka 100 na kwamba wana mkakati wa kupata waumini Milioni moja.
Pia alisema kanisa hilo lina mpango wa kufanya uinjilisti kwa kutumia njia ya teknolojia hususan mitandao ya kijamii na tayari matukio ya ibada wamekuwa wakiyaonesha mubashara kwenye akaunti yao ya Facebook inayoendana hali ya kuwashawishi vijana kuvutiwa na injili.
Katika hatua nyingine, Mchungaji Migire alisema kanisa hilo liliopo eneo la Upanga lina mpango wa kuvitembelea vyuo vilivyo karibu nalo ili kueneza injili kuhakikisha watu wanaijua Biblia pamoja na kupata waumini wapya.
Naye Katibu wa dayosisi hiyo Ndege alisema amewashukuru waumini kwa kumchagua tena kushika nafasi hiyo kwani kwake ni sehemu ya kumtumikia Mungu.
Alivitaja vipaumbele vya kanisa hilo kuwa ni ujenzi wa miundo mbinu wa huduma za jamii ikiwemo ujenzi wa shule na hospitali na tayari wamejenga Shule ya Sekondari ya Wasichana iliyopo Kigamboni pamoja na Shule ya Msingi Nyantira.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Mourice Mbunde alisema kanisa hilo linakabiliwa changamoto mbalimbali ikiwemo vijana tegemezi na kutomjua Mungu wanayemtumkia huku akisisitiza wana mpango kuandaa mafunzo ya vitendo ili kuondoa kundi la vijana tegemezi.
Post a Comment