Serikali yawashauri wakulima kuchangamkia fursa ya Bima ya Mazao, Rukwa, Ruvuma na Songwe yaongoza uzalishaji mazao ya chakula
Serikali imewashauri wakulima nchini kuchangamkia fursa ya kukata Bima ya mazao ili waweze kulipwa pale panapotokea majanga ya ukame, wadudu waharibifu na mafuriko huku ikibainisha mikoa ya Rukwa, Songwe na Ruvuma imeongoza katika uzalishaji wa mazao ya chakula.
Aidha, Serikali imesema halmashauri 44 zimeshindwa kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha na kwamba chakula kilichopo kitapelekwa katika halmashauri hizo kuondoa tatizo la chakula linaloweza kutokea.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga katika Mkutano wa Wafanyabiashara wa Nafaka wa Ndani na Nje, Wasindikaji, Wasafirishaji na Wamiliki wa Maghala.
Alisema kuwa tayari imeanzisha bima hiyo kwa kuona umuhimu wake kwa wananchi hasa kupatwa majanga yanayowarudisha nyuma kimaendeleo huku akibainisha mikoa mitatu ikiwemo ya Ruvuma umezalisha mazao ya chakula kwa asilimia 227, Rukwa asilimia 220 na Songwe asilimia 200.
“Nawashauri wakulima na wadau kuchangamkia fursa ya bima ya mazao itawasaidia kuwakinga mtalipwa kipindi ukaame, mafuriko hata wadudu wanaposhambulia mazao yenu,” alisema Waziri Hasunga.
Alibainisha kuwa Serikali imeshaanza kutumia mfumo wa Kielektroniki wa kuwasajili wakulima huku akisisitiza kuwa mchakato wa kuanzisha daftari utaazishwa kuwatambua wakulima.
Alisisitiza kuwa mkutano huo wa siku mbili utajadili namna ya kutumia mbinu bora kupata mazao ya kutosha pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kuchangamkia na kutambua fursa zilizopo.
Pia alisema katika kuhakikisha urasimu unaondolewa tayari Serikali imeanzisha mfumo wa wakulima kujisajili ili kupata leseni kwa kutumia mitandao ya simu.
Katika hatua nyingine, Waziri Hasunga amewataka wadau wa sekta hiyo kuchangamkia fursa ya kuanzisha maghala ya chakula ya kisasa ili kuisaidia Serikali kuhifadhi chakula mazingira salama na kukiuza kikiwa na ubora nje ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini, Shamte alisema bado Benki ya Kilimo inakabiliwa na changamoto ya fedha ya kutosha ya kuwakopesha wakulima na kwamba sekta hiyo ipo bega kwa bega ikiunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli kuifikisha nchi katika uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Agellah Mabula alisema kuwa wakulima wote wanaohitaji mashamba makubwa ya kufanya kilimo Serikali iko tayari kuwasaidia huku akiwataka wale wote watakaochukua maeneo kwa ajili ya kilimo kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria kwa kulipa kodi.
Post a Comment