SBL yapanda miti 1,000 Mkoani Kimanjaro kuchochea utunzaji wa mazingira
Hatua ya kuchangia katika jitihada za utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji mkoani Kilimanjaro, kampuni ya bia ya Serengeti, Serengeti Breweries Limited (SBL) kwa kushirikiana na taasisi ya The Kilimanjaro Project imezindua kampeni ya kupanda miti elfu moja mkoani humo.
Miti hiyo imepandwa katika kiwanda cha SBL kilichopo Pasua katika wilaya ya Moshi na mingine imepandwa katika wilaya ya Mwanga.
Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti, amesema SBL imeamua kuongeza jitihada za uhifadhi wa mazingira si tu katika maeneo yaliyo
chini ya SBL bali katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
“Huu ni udhihirisho tosha kwamba SBL imejidhatiti na iko tayari kushirikiana na wadau wengine katika kutekeleza miradi yenye kuleta tija kwa jamii zetu,” amesema Ocitti.
Zoezi la upandaji miti linakuja huku kukiwa na wito kutoka jumuiya ya kimataifa juu kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kuongeza juhudi za uhifadhi wa misitu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na hivyo kuyaweka mazingira katika hali ya usalama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mpango huu wa SBL unaenda sambamba na sera ya kampuni katika kurudisha kwa jamii sehemu ya faida, na umejikita zaidi katika utoaji wa huduma bora ya maji safi kupitia mradi
uitwao Water of Life (WOL); mpango kwa ajili kuwasaidia wanafunzi kupata ufadhili wa masomo ya elimu ya juu, kuwasaidia wakulima wa ndani hususani wa vijijini pamoja na mpango wa kuhamasisha unywaji pombe kistaarabu.
Zoezi la upandaji miti limehudhuriwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sara Cooke pamoja na Mwakilishi wa Waziri Mkuu wa Uingereza kitengo cha biashara, Andrew Rosindell, ambao walikuwa ziarani kiwandani hapo.
Ikiwa imeanzishwa kama Associated Breweries mwaka 1988, Kampuni ya Bia Serengeti (SBL) ni moja ya kampuni kubwa za bia nchini Tanzania, ambapo aina zake za bia zinachangia zaidi ya asilimia 20 ya bidhaa hizo katika soko.
SBL inaendesha viwanda vitatu vilivyopo Dar es Salaam, Mwanza na Moshi.
Tangu kuanzishwa kwa SBL mwaka 2002 biashara yake imekua na kuimarika zaidi na asilimia 51 ya hisa mwaka 2010 zilizochukuliwa na Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki (EABL) zimeshuhudia ongezeko la uwekezaji katika kukua zaidi na hivyo kusababisha
kuongezeka kwa fursa zaidi za ajira kwa watu wa Tanzania.
Aina za bia zinazozalishwa na SBL ambazo zimepata tuzo kadhaa za kimataifa ni pamoja na Serengeti Premium Lager, Pilsner, Tusker Lager, Tusker Lite, Kibo Gold, Guinness stout, Uhuru na Kick.
SBL pia ni wazalishaji vinywaji vikali vinavyofahamika duniani kama vile Johnnie Walker Whisky, Smirnoff Vodka, Gordon’s Gin, Captain Morgan Rum na Baileys Irish Cream.

Post a Comment