Ads

BRELA YAJIPANGA KUSHIRIKI NANENANE MKOANI SIMIYU.







Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imejipanga kikamilifu kushiriki maonesho ya nanenane kwa kutoa huduma kwa washiriki wanaotarajia kushiriki maonesho hayo ambayo yanatarajia kufanyika Mkoani Simiyu kuanzia Agosti 1-8 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Emmanuel Kakwezi, amesema  katika maonesho ya mwaka huu watatoa huduma pomoja na kuelimisha umma kuhusu namna ya kusajili kampuni na majina ya biashara.

Bw. Kakwezi amesema kuwa ni vizuri wananchi kujitokeza ili waweze kusajili biashara zao kwa urahisi katika msimu huu wa nanenane kwani wamaejipanga kutoa huduma bora katika kuhakikisha kila mshiriki ananufaika na huduma bora ya brela katika maonesho hayo.

“Brela itakuwa inatoa huduma zake palepale viwanja vya simiyu, itakuwa inatoa huduma zake zote ikiwamo kusajili makampuni, kusajili majina ya biashara, kutoa leseni, kusajili alama za biashara kutoa hati na leseni za viwanda,” amesema Bw. Kakwezi

Amesema kuwa lengo ni kuona shughuli uvuvi, kilimo na ufugaji haziishi kukidhi haja ya matumizi ya nyumbani tu, zinatakiwa ziwe shughuli za kibiashara,huku tukiendelea na utaratibu namna wanavyoweza kusajili makampuni na kuwasaidia namna ya kupata masoko.

Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda la Brela kwa sababu limesheheni wataalamu ambao watawasaidia kupata maelezo  yanayohusu huduma zinazotolewa na  Brela pamoja na kupata elimu ya kurasimisha shughuli.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, amesema kuwa Mhe. Makamu wa Rais atafungua rasmi maonesho hayo Agosti Mosi mwaka huu  na waoneshaji mbalimbali zikiwemo Taasisi, Mashirika mbalimbali na wajasiriamali wataanza kuonesha teknolojia, huduma na bidhaa zao Julai 29 mwaka huu.


“Shughuli ya ufunguzi itafanywa tarehe 01/08/2019 na Mhe. Makamu wa Rai, haya ni maonesho ambayo yatakaribisha viongozi wa Kitaifa, Agosti 03, 2019 tutakuwa na Mhe. Waziri Mkuu, Agosti 06, 2019 tutakuwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na Kilele tunatarajia kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli” amesema.


RC Mtaka amesema katika maonesho hayo wanatarajia kuwashirikisha watu zaidi ya elfu 50 ambapo pia yatawashirikisha maofisa mbalimbali wa Serikali ambao watakuwa na shughuli za kuwasaidia wananchi huku akiwataka wakulima na wajasiriamali kujitokeza kwa wingi katika maonesho haya.



Maonesho ya nanenane Kitaifa yanafanyika kwa mara ya pili mkoani Simiyu tangu Kanda ya Ziwa ilipogawanywa katika kanda mbili ambapo mwaka huu yanaadhimishwa chini ya kauli Mbiu:-“KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KATIKA UKUAJI WA UCHUMI WA NCHI”.

No comments