Mwambawahabari
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya
Uimarishaji
wa mitandao ya usambazaji mbegu na viuatilifu ni muhimu katika
kuhakikisha tija inaongezeka katika Uzalishaji wa mazao yote hususani
nafaka, matunda mbogamboga na mbegu za mafuta.
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 5 Machi
2019 wakati akizindua Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa
Mbegu na Viuatilifu, Mpango unaotekelezwa na Mradi wa NAFAKA na Kampuni
ya Kimataifa ya CORTEVA katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nchini
Tanzania.
Katika
hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya
Mhe Hasunga alisema kuwa kuimarisha usambazaji mbegu na viuatilifu
utamsaidia mkulima kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza pato lake
hivyo kuchangia katika kuipeleka Tanzania kufikia Uchumi wa Kati kama
inavyoeleza sera ya Serikali ya awamu ya tano inayongozwa na Mhe Dkt.
John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Alisema
wakulima nchini Tanzania wanategemea Sekta ya kilimo kuchangia katika
ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi, kwa kuwa inatoa ajira kwa
asilimia 65 ya wananchi, ina uwezo wa kutoa malighafi ya viwanda kwa
asilimia 66 na inachangia asilimia 100 ya chakula kinachopatikana.
Alisema
kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hiyo, Serikali kwa kushirikiana na
wadau wa maendeleo inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo
awamu ya II yaani Agricultural Sector Development Program - ASDP II inaolenga kuleta Mapinduzi katika sekta ya kilimo.
Programu
hiyo ya miaka kumi (10) imeanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2018 na
inafanyia kazi maeneo ya Usimamizi endelevu wa ardhi na maji, Kuongeza
Tija (kuongeza matumizi ya pembejeo), Kuongeza masoko na kuongeza
thamani ya mazao, Kuboresha mazingira ya uwekezaji katika kilimo. Hivyo,
Uimarishaji wa Mpango wa Kusambaza Pembejeo na Viuatilifu ni moja ya
shughuli muhimu katika Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo -ASDP 11
katika kuongeza tija.
“Ni
Imani yangu kuwa, kufanikiwa kwa kazi hii ya Mradi wa Nafaka ni
kufanikiwa katika utekelezaji wa sehemu ya Programu ya Kuendeleza Kilimo
nchini ASDP II. Mradi huu pia utaendelea kuimarisha mahusiano yaliyopo
baina na Serikali na Sekta nafsi katika kuendeleza kilimo nchini”
Alisema
Kadhalika, Hasunga alisema Serikali
inatambua mchango unaotolewa na Shirika la Misaada la Marekani USAID
katika miradi mbalimbali husasani katika sekta ya kilimo. Mradi wa
NAFAKA ni moja ya michango ya Shirika la USAID katika kuongeza tija
kupitia Mashamba darasa, Uendeshaji wa Vikundi na vyama vya wakulima,
Kuongeza thamani kwenye usindikaji wa Mahindi kwa njia ya virutubishi
kwenye unga, Kuunganisha wakulima na huduma za kifedha Masoko na Bima ya
Mazao yaani “Crop Insurance”.
Alisema kuwa Shughuli hizo zinazotekelezwa na Mradi wa NAFAKA kwa kushirikiana na CORTEVA unaenda
sambamba na jitihada za Wizara ya Kilimo katika kuendeleza kilimo. Moja
ya maeneo ya kipaumbele yanayotekelezwa na Wizara ni kuongeza tija
katika uzalishaji kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, na kuimarisha
huduma za ugani.
Maeneo
mengine ya Kipaumbele ya Wizara ya Kilimo ni Kutungwa kwa sheria ya
kilimo ili kusimamia kilimo, Kuandikisha wakulima wote, Kuongeza
uzalishaji wa sukari kuondoa upungufu wa sukari nchini, Kufungamanisha
uzalishaji na mahitaji ya viwanda ili kutoa mali ghafi ya viwanda kwa
kuongeza uzalishaji, Kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta, Kuanzisha
scheme za umwagiliaji ili kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji,
Wakulima kuwa na bima ya mazao, na Kuongeza fursa za upatakanaji wa
fedha kwa wakulima.
“Ni
jambo la faraja kuona sekta binafsi sasa zinatoa mchango katika
jitihada za Serikali katika kutoa mafunzo kwa wakulima kwa kuanzisha
mashamba darasa, kutoa mafunzo kwa maafisa ugani, kusimamia na kuhimiza
matumizi ya mbegu bora na viuatilifu pamoja na kufanya kazi na mawakala
wa pembejeo wa daraja la kati na wadogo waliopo vijijini wapatao”
Alikariirwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa
“Ni
jambo la kutia moyo kuwa mpango huu utasaidia usambazaji na upatikanaji
wa viuatilifu vya kupambana na visumbufu vya mlipuko vikiwemo viwavi
jeshi vamizi “Fall Army Worms” katika maeneo yaliyovamiwa kwenye Mikoa
ya Nyanda za Juu Kusini nchini mwetu”
Aidha,
alisema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika
kilimo ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio katika taratibu zilizowekwa
katika uzalishaji, usambazaji na uingizaji wa mbegu ili kurahisisha
upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima nchini.
Katika
suala la soko la mahindi Serikali imesharekebisha suala hil0 na
itaendelea kutoa taarifa za hatua zinazochukuliwa na Serikali katika
kuboresha taratibu za masoko ya mazao ili wakulima, wafanyabiashara na
wadau waweze kunufaika na uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Sambamba
na hayo pia Waziri Hasunga alisema kuwa serikali itaweka msisitizo
katika sekta ndogo ya ardhi ili wakulima kuona umuhimu wake na
kuondokana na kilimo kinachotegemea mvua.
Post a Comment