Serikali Yazidi Kuimarisha Mazingira ya Uwekezaji

Na Grace Semfuko-MAELEZO
Serikali
imeweka mpango wa kuboresha mazingira ya Biashara na uwekezaji kwa
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi mpango unaolenga kurahisisha vibali
na upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Viwanda na maeneo ya
Kilimo.
Hayo
yamebainishwa Jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki wakati akizungumza na Waandishi wa
Habari kwenye makao makuu ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, baada ya
kupokea ujumbe wa raia saba wa Hongkong China waliowasili Nchini
wakiwawakilisha wafanyabiashara wa nchi hiyo waliokuja kufanya utafiti
wa maeneo ya kuwekeza.
Waziri
Kairuki alisema hivi sasa Wizara yake iliyopo Chini ya Waziri Mkuu
imeanza kuufanyia kazi mpango huo ambapo pamoja na kuimarisha uchumi wa
Nchi kwa kuingiza fedha za kigeni pia utaongeza ajira kwa watanzania.
“Sisi
kama Serikali lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunaimarisha uwekezaji,
mpango huo ambao ulifanyika mwezi Mei mwaka jana unalenga kuondokana na
vikwazo vya kibiashara na kuharakisha vibali na kutoa ardhi kwa ajili ya
uwekezaji, tunayafanya haya ili kuongeza ufanisi katika sekta ya
uwekezaji, tunataka Watanzania wanufaike” alisema Angellah Kairuki.
Alisema
mwaka 2018 mwezi Mei Serikali iliweka mkazo katika andiko la mpango wa
kuboresha biashara na uwekezaji pamoja na mpango mkakati wa
kuhakikisha kuondoa vikwazo vya biashara mpango ambao unafanikiwa kwa
kiwango kikubwa.
Nae
Jessica So ambaye ni Mwakilishi wa Balozi wa Heshima wa Tanzania
Hongkong alisema lengo la ujio wao ni kufanya utafiti wa maeneo ya
uwekezaji na kibiashara ambapo wanaanza kwa kuangazia maeneo manne
yaliwepo ya Sekta ya Dawa, Kilimo cha Ufuta na Korosho pamoja na Sekyta
ya Utalii.
“Sisi
ni ujumbe wa watu saba kutoka Hongkong China, tumekuja hapa kuangalia
ni kwa namna gani tutashirikiana na Tanzania katika kuwekeza kwenye
maeneo manne ya Dawa, Ufuta,Korosho na Utalii, tunawawakilisha
wafanyabiashara wengine na tutawapelekea ujumbe wa tutakayoyaona hapa
Tanzania” alisema Mwakilishi wa Wajumbe hao Jessica So Raia wa HongKong
China.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Geoffrey Mwambe alisema
tayari walishafanya mazungumzo na Mamlaka ya maendeleo ya biashara
Hongkong ambayo inashughulikia biashara na uwekezaji kusaini makubaliano
ya kuhakikisha wafanyabiashara wengi wanatumia fursa zilizopo Hongkong
na Tanzania.
Post a Comment