Waziri Lugola Kuanza Ziara Ndefu Mkoani Arusha Kesho Kufuatilia Maagizo Yake
Na Felix Mwagara, MOHA-Arusha.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewasili jijini Arusha leo,
kwa ajili ya kuanza ziara yake ya kikazi ya siku kumi kwa kutembelea
Wilaya zote za Mkoa huo akisikiliza kero za wananchi pamoja na
kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama
vilivyopo ndani ya Wizara yake.
Waziri
Lugola anatarajia kuanza ziara hiyo rasmi kesho Februari 13, 2019
jijini humo kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa na kupokea taarifa ya Kamati hiyo, kabla ya kuanza
kuzungumza na Wakuu wa vyombo vyake na baadaye atakutana na Kamati ya
Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa, na kumaliza kwa kuzungumza na
Baraza la Askari na Watumishi wote wa Wizara hiyo waliopo jijini humo.
Akizungumza
na Mwandishi wa habari hii, leo, Lugola amesema baada ya kuzungumza na
Askari na Watumishi wa Wizara yake pamoja na kupokea changamoto zao,
atafanya mkutano mkubwa wa hadhara wa wananchi utakaofanyika katikati ya
Jiji hilo ili wananchi wengi waweze kufika kwa wingi na aweze
kusikiliza kero zao na Waziri huyo kuweza kuzitatua.
“Nitafanya
mkutano mkubwa wa hadhara katika jiji la Arusha, ambapo utaanza saa
10:00 hadi 12:00 jioni, hivyo nawaomba wananchi wa Jiji hili wajitokeze
kwa wingi kunisikiliza kile ambacho nimepanga kuwaambia na pia nitawapa
nafasi wananchi waulize maswali bila woga, waniambie kero zao nami
nitazitatua katika mkutano huo,” alisema Lugola.
Pia
Lugola alisema lengo la ziara hiyo ni kufuatilia maagizo yake
mbalimbali ambayo aliyatoa mwaka jana 2018 katika mikutano yake kama
yalifanyiwa kazi na viongozi wa Taasisi anazoziongoza au yalipuuzwa,
yakiwemo ya dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi
nchini, na pia kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia
kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni
ziondolewe.
Lugola
alisema katika ziara yake aliyoifanya mwaka jana Mkoani Kigoma na mwezi
Januari Mwaka huu Mkoa wa Kagera, aligundua wananchi wanakabiliwa na
changamoto mbalimbali hivyo hawezi kulala akiwa ofisini, lazima afanye
ziara nchi nzima kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo wengi wao
wakiwalalamikia Polisi wakiwaonea.
Waziri
Lugola ameongeza kuwa, kupitia mikutano yake ya wananchi mkoani Kigoma
na Kagera ndipo ameamua kufanya ziara ya tatu kwa kuutembelea Mkoa wa
Arusha ambao changamoto zake zinafanana kwa sehemu kubwa kwa kuwa mikoa
hiyo ni ya mipakani na changamoto kubwa ni uwepo wa wahamiaji haramu
pamoja na matukio kadhaa ya ujambazi ambayo kwa kiasi kikubwa Serikali
inaendelea kuyadhibiti.
“Wananchi
wanapojitokeza kwa wingi inasaidia kusikiliza matatizo yao
yanayowakabili, ndio mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima,
hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na
kuangalia utendaji kazi wa Taasisi zangu zilizopo ndani ya Wizara hii,
na hakika Serikali ya Rais Dokta John Magufuli inawajali wananchi wake
ndio mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na Serikali yao uso
kwa uso,” Alisema Lugola.
Waziri
Lugola baada ya kumaliza ziara yake Jijini Arusha, ataenda Wilaya ya
Arusha ambayo itakua Februari 14, Meru Februari 15, Arumeru, baadaye
Longido, Monduli, Karatu na ataimaliza ziara yake akiwa Wilaya ya
Loliondo mkoani humo.
Katika
Wilaya zote atakazozitembelea pia atazungumza na wananchi pamoja na
watumishi waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara
ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu
lake kuu ni kupunguza msongamano gerezani na kusimamia wafungwa
waliopewa adhabu mbadala na Mahakama au wafungwa waliopata msamaha
kupitia sheria ya huduma kwa jamii na kutumikia kifungo chao nje ya
Gereza.
Post a Comment