MHE.MKUCHIKA APONGEZA WANUFAIKA WA TASAF WA KIJIJI CHA MKWANYULE WILAYANI KILWA KWA KUTUMIA VIZURI FEDHA ZA TASAF KUJIKWAMUA KIUCHUMI
Mwambawahabari
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb)
amepongeza jitihada za Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
(TASAF) wa kijiji cha Mkwanyule wilayani Kilwa za kujikwamua kiuchumi
kwa kutumia vizuri fedha za TASAF.
Pongezi hizo amezitoa wakati wa mkutano kati yake na wakazi wa kijiji cha Mkwanyule wilayani Kilwa uliofanyika kwenye viwanja vya shule
ya msingi Mkwanyule wilayani humo.
Mhe. Mkuchika ametoa pongezi hasa kwa kinamama kwa kutumia vizuri
fedha hizo katika kuzalisha miradi ya maendeleo na amefurahishwa na
ushuhuda wa akina mama ambao mwanzoni walitumia vibaya fedha hizo lakini
baadae wakawekeza katika miradi ya maendeleo.
Mhe. Mkuchika ametoa ufafanuzi kuwa lengo la kuanzishwa kwa TASAF
ni kupambana na umaskini ili kuboresha hali duni za Watanzani na kuagiza
wanufaika wa TASAF kutofanyia mzaha fedha wanazozipata.
Aidha, Mhe. Mkuchika amepongeza wasimamizi wa TASAF katika Halmashauri
ya Wilaya ya Kilwa akiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Mratibu wa
TASAF wa halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi
ya TASAF.
Akitoa ushuhuda katika mkutano huo, mmoja wa wanufaika wa TASAF mkazi
wa kijiji cha Mkwanyule, Bi. Mwanahamisi Ukwenda, ameishukuru serikali
kwa kuianzisha TASAF kwani imemuwezesha kufanya shughuli za ufugaji
wa kuku na mbuzi na kupata fedha ambazo zinamsaidia kwa mahitaji maalumu
mara anapouza mifugo hiyo.
Aidha, Bi. Mwanahamisi amekiri kutotumia vizuri fedha za TASAF alizozipata
katika awamu ya kwanza na ya pili na kuahidi kuendelea kuzitumia vizuri
fedha hizo kwa sasa.
Mnufaika mwingine, Bw.Hassan Charahani ameushukuru mradi
wa TASAF kwa kumkwamua kwenye umaskini kwani hapo awali alikuwa akila
mlo mmoja kwa siku na hakuweza kusomesha watoto lakini TASAF imebadili
maisha yake.
Kwa upande wake Mbunge wa Kilwa Kusini,
Mhe. Selemani Bungara ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuwezesha wakazi wa kijiji cha Mkwanyule kuwa na miradi
ya ufugaji kuku, mbuzi na kujenga bwawa la maji na pia ameipongeza serikali
kwa kutokua na ubaguzi katika kuleta maendeleo nchini kwa kuwa Mkwanyule
inaongozwa na viongozi wa chama cha CUF.
Mhe. Mkuchika anaendelea na ziara
ya kikazi mkoani Lindi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi
wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.
Post a Comment