WAZIRI MKUU ANUSA UFISADI UKARABATI WA JENGO SONGEA
Ni la wajawazito wanaosubiri kujifungua, limegharimu sh. milioni 129
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amenusa
harufu ya ufisadi katika mradi wa ukarabati wa jengo la mama na mtoto
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma (HOMSO) na amesema kwamba
hajaridhishwa na kiasi ya sh. milioni 129 zilizotumika.
Hivyo,
amemuagiza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
Dkt. Faustine Ndungulile afuatilie suala hilo ili kumbaini mtu ambaye
amehusika katika kupitisha zabuni ya ukarabati wa jengo hilo na kisha
kumpelekea taarifa.
Waziri
Mkuu amenusa harufu ya ufisadi katika mradi huo leo (Jumamosi, Januari
5, 2019) wakati alipotembelea hospitali hiyo na kukagua ukarabati wa
jengo la akinamama wajawazito wanaosubiri kujifungua (mama ngojea)
ambalo umegharimu sh. milioni 129.
“Sijaridhishwa
na gharama za ukarabati wa jengo hilo kutokana na kiasi kikubwa cha
fedha kilichotumika kwani Serikali inajenga vituo vya afya vyenye jengo
la maabara, jengo la kujifungulia, wodi ya mama na mtoto, chumba cha
upasuaji, nyumba ya watumishi kwa gharama za sh. milioni 400 hadi 500
sasa inawezekajane jengo moja linalokarabatiwa ligharimu kiasi hicho.”
Waziri
Mkuu amesema kila mtumishi wa umma lazima azingatie maadili ya
kiutumishi na kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na Serikali.
Amesema Serikali imeagiza miradi ijengwe kwa kutumia force accountna kuhakikisha miradi inalingana na thamani ya fedha.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia kikamilifu
utoaji wa huduma ya watoto waliochini ya miaka mitano zinazotolewa
katika hospitali kwani baadhi ya wahudumu wa afya wamekuwa wakiwatoza
gharama za dawa wakati wanatakiwa watibiwe bure.
Waziri
Mkuu amesema hayo baada ya Kanisia Fusi ambaye amelazwa na mtoto wake
katika hospitali hiyo kumueleza kwamba ameandikiwa dawa na kuambia
akanunue wakati mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu anatakiwa
atibiwe bure.
Pia
baada ya Dkt. Ndungulile kuangalia cheti cha mtoto huyo alisema dawa
aliyoandikiwa ipo hospitalini hapo jambo ambalo lilithibitishwa na
Mganga Mfawidhi wa hopitali hiyo Dkt. Majura Magafu, hivyo Waziri Mkuu
amemuagiza mganga huyo amtafute mtendaji aliyemuambia mama huyo
akanunue.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amezindua mpango wa usambazaji wa x-ray za kidigitali
ambazo zitazambazwa kwenye hospitali mbalimbali za rufaa za mikoa ili
kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa kwa njia ya mionzi.
Waziri
Mkuu amesema kwa kuanzia x-ray hizo zitasambazwa kwenye hospitali za
rufani katika mikoa 11 na kisha baadae zitasambazwa kwenye hospitali
zingine 20, lengo ni kuhakikisha hospitali zote za rufaa za mikoa
zinakuwa na x-ray hizo.
Kwa upande wake,
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt.
Ndungulile amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.
John Magufuli imeendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha huduma za
nchini.
Amesema
lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Watanzania
wote karibu na maeneo yao ya makazi tena kwa gharama nafuu. ”Katika
kufikia azma hii moja wapo ya kipaumbele ni kununua vifaa vya kisasa
vinavyoendana na teknolojia iliyopo.”
Amesema
kwa sasa wizara hiyo imenunua mashine 11 za x-ray za kidigitali zenye
thamani ya zaidi ya shilingi 2,027,029,794.60 ambazo zimekusudiwa
kupelekwa kwenye hospitali 11 zenye x-ray za zamani. Hospitali hizo ni
Amana, Bukoba, Katavi, Morogoro, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Singida na
zingine tatu zitafungwa katika hospitali za wilaya za Chato, Magu na
Nzega.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JANUARI 5, 2019.
Post a Comment