Serikali Kuajiri Walimu Wapya 6000 Mwaka Huu

Na Mathew Kwembe, Chemba, Dodoma
Serikali
imesema kuwa mwaka huu inatarajia kuajiri walimu wapya 6000 wa masomo
ya Sayansi na Hesabu ambapo tayari kibali cha kuwaajiri walimu hao
kimekwishatolewa.
Aidha
Serikali inakusudia kuwapeleka walimu 11,000 wa masomo ya sanaa ambao
ni wa ziada waliokuwa wakifundisha shule za sekondari kufundisha shule
za msingi ili kukabiliana na upungufu wa walimu unaozikabili shule za
msingi nchini.
Naibu
Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
anayeshughulikia elimu Mhe.Mwita Waitara ameyasema hayo jana katika
Wilaya Chemba, mkoani Dodoma wakati akizungumza na watumishi kutoka
Idara za Elimu ya Msingi na Sekondari kutoka Halmashauri hiyo.
Kauli
hiyo ya Serikali inafuatia taarifa ya Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri
ya wilaya ya Chemba bwana Josephat Ambilikile kumweleza Naibu Waziri
kuwa Halmashauri ya Chemba ina upungufu wa walimu 808 kati ya walimu
1628 wanaotakiwa kufundisha katika shule za msingi 103 zilizopo katika
wilaya hiyo.
Mhe.Waitara
alisisitiza kuwa Serikali kuanzia mwaka huu itakuwa ikiajiri walimu
kila mwaka ili kufidia walimu wanaostaafu na pia kukabiliana na upungufu
unaotokana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule za msingi
kutokana na mwitikio wa wazazi kupeleka watoto wao shule kufuatia uamuzi
wa serikali ya awamu ya tano kutoa elimu ya bila malipo.
“Tayari
Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli amekubali walimu waajiriwe na
kibali kimekwishatolewa hivyo walimu 6000 wa masomo ya sayansi na hesabu
na pia walimu 11,000 ambao ni walimu wa ziada waliokuwa wakifundisha
masomo ya sanaa katika shule za sekondari watapelekwa kufundisha shule
za msingi,” alisema Mhe.Waitara.
Pamoja
na kueleza juhudi hizo za serikali za kuongeza idadi ya walimu, Naibu
Waziri aliwataka walimu wanaofundisha masomo ya sayansi na hesabu
kutowakatisha tamaa wanafunzi wanapowafundisha wanafunzi masomo hayo
badala yake watumie mbinu rahisi ili wanafunzi waelewe kwa urahisi
masomo hayo.
“Tunatarajia Walimu wanapaswa kutumia mbinu rahisi wanapofundisha hesabu ili wanafunzi wapende somo hilo,” alisema na kuongeza:
“Hata
utunzi wa vitabu vya kufundishia masomo hayo inabidi uangaliwe upya
kwani watoto wanakimbia kusoma masomo ya sayansi na hesabu kwani
kutokana na namna vitabu hivyo vinavyotungwa vinasababisha watoto
wachukie masomo ya sayansi na hesabu,” alisema Waitara.
Jambo
lingine alilolizungumzia Naibu Waziri ni kiwango duni cha ufaulu
kilichoonyeshwa na Mkoa wa Dodoma hasa wilaya ya Chemba katika matokeo
ya kitaifa ya darasa la saba na kidato cha nne ambapo aliwataka
watendaji wa elimu katika halmashauri hiyo kuja na mikakati
itakayoboresha elimu wilayani humo.
“Ukitaja
wilaya 10 zilizofanya vibaya kwa ufaulu Chemba ni ya 10 kwa matokeo ya
darasa la saba, mkae chini mje na mkakati wa kuboresha matokeo ya wilaya
yenu, cha muhimu mikakati hiyo ishirikishe ngazi zote kuanzia ngazi ya
mkoa, wilaya, tarafa hadi kata,” alisema.
Pia
Naibu Waziri alikemea tabia iliyojitokeza hivi karibuni kwa baadhi ya
watendaji wa elimu kushiriki katika kuiba mitihani ambapo aliagiza kuwa
kama kuna mwalimu ameshiriki katika wizi wa mitihani halmashauri isisite
kumchukulia hatua kwani kitendo hicho kinarudisha nyuma maendeleo ya
elimu ya nchi.
Sambamba
na hilo Mhe.Waitara alionya tabia ya baadhi ya watendaji wasio
waaminifu katika halmashauri kutumia kinyume na maelekezo ya serikali
fedha za miradi kwa ajili ya kusaidia miundombinu ya shule.
“Fedha
kama ni kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ipokee na iende ikajenge
hosteli, kadhalika kama fedha ni kwa ajili ya kununulia samani za shule
ipokee na iende ikanunue samani za shule, ukigusa fedha ya elimu kinyume
na maelekezo ya serikali tutashughulika na wewe,” alionya Waitara.;
Mapema
Naibu Waziri alipata fursa ya kutembelea shule ya sekondari na shule ya
msingi ya Chemba na kushuhudia ujenzi unaoendelea wa chumba kimoja cha
darasa katika shule ya sekondari chemba, ujenzi ambao umetokana na
michango ya wananchi.
Post a Comment