Zitto Kabwe 'Kujisalimisha' TAKUKURU Kesho Ijumaa
Kiongozi
wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kesho anatarajia kuitikia wito
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuhusiana na
mambo aliyoandika kwenye mitandao ya kijamii.
Takukuru
kupitia Naibu Mkurugenzi Mkuu wake, Brigedia Jenerali John Mbungo,
ilimtaka kiongozi huyo kufika ofisini kwake kutoa ushahidi wa tuhuma
alizozitoa kuwa kuna kampuni tatu za chuma zimewahonga baadhi ya
viongozi wa serikali.
Sehemu
ya taarifa ya wito huo ilieleza kuwa: “Tunatoa taarifa hii kupitia
vyombo vya habari kumwomba Zitto Kabwe afike ofisi za Takukuru Dar es
Salaam mapema iwezekanavyo ili tushirikiane katika kulishughulikia suala
hili muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.”
Alipotafutwa
Afisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis, kueleza ni lini
kiongozi huyo atakwenda kuripoti Takukuru, alisema Zitto ataripoti
Takukuru Ijumaa (kesho).
Kwenye
mitandao ya kijamii Zitto alidaiwa kuandika kuwa amepata habari za
kushtusha kuwa kampuni tatu za China, Russia na Uturuki zimewahonga
baadhi ya watendaji wa serikali kuchelewesha mradi wa Mchuchuma na
Liganga. Lengo ni kuhakikisha nchi hizo zinapata soko la chuma chao.
Aliendelea
kuandika kuwa kuhujumu mradi wa Mchuchuma na Liganga ni uhaini. Baadhi
hawawezi kusahau hujuma hiyo na yeyote anayeshiriki atasakwa mpaka
kaburini kwake, ikibidi kuondoa kinga za watu ili liwe fundisho kwa
uhujumu huu uchumi na uhai wa taifa letu.
Aliandika
zaidi kuwa msamaha wa kodi kwa bomba la mafuta kutoka Uganda ni mkubwa
na hauna faida kulinganisha na mradi wa Mchuchuma na Liganga utakaotoa
ajira za kudumu 35,000 kuingiza fedha za kigeni bilioni 4.6 kwa mwaka na
kuifanya nchi yetu kuwa na viwanda vikubwa.
Post a Comment