Ads

WAZIRI MKUU AAGIZA VYOO NA MIFUMO YA MAJI VIWANDANI IKAGULIWE

Mwambawahabari
.............................
*Asisitiza vitakavyobainika kuwa na makosa hatua kali zichukuliwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi na Ajira ifanye ukaguzi wa vyoo na mifumo ya kutiririsha maji katika viwanda vyote na vitakavyobainika na makosa hatua kali zichukuliwe.

Pia, Waziri Mkuu amewaagiza maafisa afya na mazingira katika mikoa yote nchini badala ya kuzingatia maeneo ya hoteli, mabucha na migahawa waende kwa jamii na kutoa elimu ya matumizi ya vyoo bora pamoja na umuhimu wa usafi wa mazingira, hivyo watakuwa wameiepusha na maradhi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Novemba 23, 2018) kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Usafi wa Mazingira Kitaifa na Mkutano wa Maafisa Afya wa Mikoa, Halmashauri na Wadau wa Afya Mazingira Tanzania, uliofanyika jijini Dodoma.

Amesema viwanda vina jukumu la kuhakikisha vinatunza afya za wafanyakazi wake kwa kufuata taratibu na sheria za afya kazini. “Ni jukumu la kila kiwanda kuhakikisha kwamba kinadhibiti uchafuzi wa hewa ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”

Amesema kwamba hivi sasa, madhara ya mabadiliko ya tabianchi yameanza kushuhudiwa  nchini na endapo jitihada za makusudi zisipochukuliwa ipo hatari ya kufifisha matarajio ya kesho na kesho ya watoto. 

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu ametoa rai kwa wakuu wote wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na maafisa watendaji wa kata, mitaa na vijiji nchini kwamba wasimamie vizuri na kwa ukaribu kampeni ya usafi wa mazingira na matumizi ya choo bora.

“Hakikisheni kuwa lengo la kila kaya nchini kupata choo bora kabla ya tarehe 31 Desemba, 2018 linafikiwa. Waziri mwenye dhamana, tambua kwamba baada ya tarehe husika kupita nitahitaji kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa agizo hilo kutoka kwa kila mkoa na halmashauri nchini.” 

Waziri Mkuu amesema ameelezwa kwamba, hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2018 kaya zenye vyoo bora zimefikia asilimia 51.4 kutoka asilimia 46.6 Julai, 2017 na katika kipindi hicho kaya zisizokuwa na vyoo kabisa imepungua kutoa asilimia 5.4 hadi asilimia 3.8. 

Amesema iwapo watazidisha kasi katika utoaji wa elimu, usimamizi wa sheria na kuongeza ufuatiliaji, kaya zote zitakuwa na vyoo bora ndani ya muda mfupi ujao. “Nimedokezwa hapa kwamba, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika hilo. Sasa nitashangaa sana kwa nini wengine mshindwe?

Sambamba na suala hilo la ujenzi na matumizi ya vyoo bora katika kaya, pia Waziri Mkuu amesisitiza uwepo wa huduma za vyoo bora kwa taasisi zote za umma na binafsi. “Ninaagiza shule zote, vituo vyote vya tiba, vituo vya abiria, masoko na nyumba zote za ibada ziwe na miundombinu bora ya vyoo na sehemu za kunawa mikono.” 

Kadhalika, Waziri Mkuu amewagiza wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe maeneo yote hayo yanakuwa na huduma hizo muhimu kabla ya tarehe 30 Aprili, 2019 ili itasaidia sana kuondokana na aibu ya kukosa miundombinu ya usafi katika taasisi zao. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameonya jamii dhidi ya tabia ya ya kuchimba dawa wakati wa safari. “Tabia hii imeota mizizi, imekuwa kama ni desturi ya baadhi ya watu licha ya Serikali pamoja na sekta binafsi imeweza kuweka huduma za vyoo kwenye stendi za mabasi, vituo vya kuuzia mafuta, pamoja na hoteli zinazotumiwa na wasafiri.” 

Amesema haiingii akilini kuona basi la abiria linasimama porini ili watu wajisaidie wakati muda mfupi uliopita basi hilo lilisimama kwenye kituo kikubwa cha abiria au sehemu zinazotoa huduma ya chakula.

“Katika kudhibiti hali hii ninaagiza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani, SUMATRA na TABOA kuandaa mikakati ya kuondokana kabisa na tabia hii hatarishi kiafya. “

Waziri Mkuu amewaagiza maafisa afya mazingira kote nchini watekeleze wajibu wao kwa kuwachukulia hatua za kisheria madereva na makondakta wote watakaobainika kusimamisha magari porini kwa lengo la kuchimba dawa.

Katika mkutano huo halmashauri ya wilaya ya Njombe imeibuka kidedea kwenye kundi la utekelezaji wa kampeni ya Taifa ya usafi wa mazingira, ambapo imepewa zawadi ya gari aina ya ford ranger lenye thamani ya Dola za Marekani 35,700.

Mbali na halmashauri hiyo kuibuka mshindi na kupata zawadi ya gari jipya pamoja na tuzo, ndiyo Halmashauri pekee nchini ambayo kaya zake zote zina vyoo bora na kwamba hakuna kabisa tabia ya kujisaidia vichakani. 

Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa halmashauri nyingine nazo ziige mfano huo wa Njombe. “Ni dhahiri kuwa endapo halmashauri zote zitafikia hadhi ya Njombe tutaokoa fedha nyingi ambazo zinatumika kugharamia matibabu ya wagonjwa pamoja na kuokoa muda mwingi unaohitajika kwenye shughuli za uzalishaji ambao unapotea kila siku kwa kuuguza watu wanaopata magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya uchafu.” 

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
  S. L. P. 980,
 41193 – Dodoma,                       
IJUMAA, NOVEMBA 23, 2018.

No comments