Ads

DKT. NDUGULILE – “SEKTA YA AFYA NCHINI INAKUWA KWA KASI”

Mwambawahabari
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akionyesha mafuta maalum kwa ajili ya kuwakinga wenye ulemavu wa ngozi dhidi ya miale ya jua yanayotengenezwa na  kitengo cha Kilimanjaro Sunscreen Production kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC.
..............................................................
“Sekta ya afya inakua kwa kasi huku huduma muhimu za afya kwa sasa zikiwa zinapatikana hapa hapa nchini”

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile alipokua akizungumza na watumishi wa Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) iliyopo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro jana Novemba 22, 2018.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa Sekta ya Afya imepewa kipaumbele cha hali ya juu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli katika kipindi cha miaka mitatu mageuzi makubwa ndani ya sekta ya afya yameanza kuonekana huku huduma za matibabu ya kibingwa yakiwa zikipatikana hapa hapa nchini.

“Tunasimama hapa kifua mbele tukiona mabadiliko katika hali ya upatikanaji wa dawa kuimarika zaidi, bajeti ya dawa imeongezeka toka Shilingi Bilioni 30 mpaka Shilingi Bilioni 270 yaani mara tisa zaidi ndani ya miaka mitatu” alisema Mhe.Naibu Waziri na kuendelea “Tumeboresha vituo vya afya takribani 300, huku Mkoa wa Kilimanjaro ukiwa na Vituo 8 vilivyoboreshwa vilivyogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 3.5 na kwa mwaka huu 2018 Serikali imeanza kujenga Hospitali za Wilaya 67 nchini”

Aidha, Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali imetenga Shilingi Bilioni 30 kwa ajili ya Hospitali mpya za Rufaa za Mikoa ili  ziweze kutoa huduma za kibingwa, kupunguza msongamano wa wagonjwa na ucheleweshwaji wa huduma katika Hospitali za rufaa za kanda.

Naibu Waziri huyo Aliendelea kusema  kuwa fedha hizo Shilingi Bilioni 30 zitaelekezwa katika maeneo makuu matano ambayo aliyataja kuwa ni kuhakikisha kila Hospitali ya Mkoa ina Kitengo cha dharura, chumba cha upasuaji, kitengo cha uangalizi wa wagonjwa mahututi pamoja na kitengo cha mama na mtoto.

"Hospitali hii inatakiwa kuhudumia wagonjwa waliopata rufaa toka hospitali za mikoa ya jirani waje huku kupatiwa huduma za matibabu na sio wagonjwa wa malaria na mafua alisema Dkt. Ndugulile.

Katika kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa kwenye hospitali za rufaa za mikoa, Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imeweka maeneo muhimu katika mafunzo kwa watumishi wa kada ya afya huku akitaja watumishi wenye kuhitajika zaidi kwa sasa kuwa ni madaktari wa magonjwa ya ndani, watoto, wakina mama, upasuaji, mifupa pamoja na madaktari wa usingizi.

Kuhusu upatikanaji wa huduma za kibingwa, Dkt.Ndugulile alisema  mafanikio  kuona huduma hizo zikiwa zinapatikana hapa nchini tofauti na zamani  “Tunafanya upandikizaji wa figo pamoja na upandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa wa watoto huduma ambazo zilikuwa ni za kufikirika ndani ya miaka mitatu sasa zinapatikana hapa nchini” alisema Dkt. Ndugulile.

Awali akitoa taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC Dkt. Gileard Masenga aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Hospitali hiyo "Licha ya kumilikiwa na Taasisi ya kidini lakini Serikali imeendelea kutupatia wataalam, misamaha ya kodi za malighali zinazoingizwa nchini ambazo hutumika kutengeneza mafuta ya kuwakinga wenye ulemavu wa ngozi dhidi ya jua.

Aidha, Dkt.Masenga alisema hospitali yake imetengewa  Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya dawa za Saratani huku fedha kiasi cha Shilingi Milioni 250 tayari  zimeshapelekwa Bohari ya dawa kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo.

 Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto yupo Mkoani hapa kwa ziara  ya kikazi  inayolenga kukagua shughuli za huduma ya Afya,Maendeleo ya Jamii pamoja na kuongea na watumishi wa sekta  hizo.

No comments