WAMASAI SIMANJIRO WATAKIWA KUACHA KUWATUMIA WATOTO WA KIKE KAMA BIDHAA.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akipanda mti mara baada ya kuzindua Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji Orkesumet Simanjiro Mkoani Manyara.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile pamoja na Laigwenani wa Kimasai Mzee Maika Ngukuu (84) wakizindua Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji cha Shirka la NAFGEM kilichopo Orkesumet Simanjiro mkoani Manyara.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akionesha kufuraishwa kwake na
baadhi ya bidhaa za wanawake
wajasiliamali wakimasai wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji
Orkesumet Simanjiro Mkoani Manyara .
Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
Na Anthony Ishengoma - Manyara
Jamii ya Wamasai nchini imetakiwa kuacha tabia ya
kumtumia mtoto wa kike kama bidhaa na kuanza kuwapeleka watoto wakike shuleni
badala ya kuwaozesha wakiwa wadogo kama mtaji wa kujipatia ng’ombe.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile aliyasema
hayo jana alipofanya ziara ya siku moja Wilayani Simanjiro kwa aijili ya
kukagua hospitali lakini pia kuzindua Kituo cha Mtandao wa Kupinga Ukeketaji
kilichopo Makao Makuu ya Wilaya ya Simajiro eneo la
Orkesumet.
Dkt. Ndugulile aliongeza kuwa ni muhimu kwa Wamasai
kuanza kujenga jamii inayoelimika ili kuweza kutokomeza baadhi ya mila
zisizofaa kwani jamii ikielimika baadhi ya mila na desturi katika jamii husika upotea zenyewe.
Awali Mkurugezi Mtendaji wa Kituo cha Mtandao wa
Kupambana na Ukeketaji Simanjiro Bw. Francis Selasini alimwambia Dkt. Ndugulile
kuwa kituo chake kilimwokoa mtoto wa miaka minane ambaye alikuwa anakaribia
kuolewa na mzee wa miaka 72 ambaye tayari alishakubaliana na wazazi wake kumuoa
na mtoto huyo kwa sasa amemaliza darasa la saba kwa msaada wa kituo hicho.
Dkt. Ndugulile aliwaambia Wazee wa Kimila kutambua kuwa ni
kinyume na matakwa ya serikali na ni dhambi kubwa kuozesha watoto wadodo
hususan watoto walio chini ya miaka kumi na nane akiitaka jamii hiyo kubadilika
na kuelimisha watoto wa kike kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
Naibu Waziri Ndugulile pia amemtaka Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhandisi Zephania Chaula
kuwezesha wanawake wa kimasai kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ili waweze
kuzalisha mali kama hatua ya kupambana na umasikini kwani wanaume wao mara
nyingi uhama na mifugo yao na kuacha na mzigo mkubwa wa kutunza familia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mtandao Kupambana
na Ukeketaji cha NAFGEM Simajiro Bw.Francis Selasini katika ya hotuba yake kwa Naibu
Waziri Ndugulile alisema wakeketaji kwa sasa wamebadili mbinu ya ukeketaji na
kwasasa wanakeketa watoto wadogo kwa nyakati za husiku kwa sababu watoto hao
hawana uwezo wa kutoa taarifa.
Hii hii inatokana na serikali pamoja na wadau kupinga
vitendo vya ukeketaji lakini Mkurugenzi huyo pia amepinga takwimu zilizopo
zinazosema mkoa wa Manyara una asilimia 58 ya vitendo vya ukatili hapa Nchini.
"Takwimu zinaonesha Mkoa wa Manyara una asilimia 58 ya
vitendo vya ukatili hapa nchini lakini takwimu hizi hazioneshi uhalisia kwa
kuwa Mkoa huu jamii zake zote zina mila ya ukeketaji na vitendo hivi vipo kwa
wingi sana tunaomba serikali itoe njia bora ya utafiti ili tuwezo kujua
kiuhalisia ukubwa wa tatizo.” Alisema Bw. Selasini.
Akihitimisha hotuba yake kituoni hapo Naibu Waziri
Ndugulile aliyataka Mashirika ya SIDO, TFDA, na mengine Wilayani humo kutoa
elimu ya namna bora ya kutengeneza bidhaa zenye ithibati ili bidhaa za
wajasliamali wanawake ziweze kushindana kwa ubora katika Soko.
Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji cha NAFGEM kilichopo Wilaya ya Simanjiro
kimekuwa msaada Mkubwa kwa Jamii ya Kimasai kwani kwa sasa kinawatunza
Wasichana wanaokimbia ukeketaji na kuwarudisha shuleni na wengine kuwafundisha
ujasiliamali wa kutengeneza sabuni, batik na ushonaji pamoja na shule ya
chekechea kwa watoto wadogo.
Post a Comment