NEMC IMULIKE UTEKELEZAJI WA SHERIA YA MAZINGIRA MIRADI YA UWEKEZAJI
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
SEKTA zote za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, maji
na nishati zinategemea mazingira kama rasilimali muhimu katika kuchangia
ukuaji wa uchumi wa nchi.
Hata hivyo, shughuli zisizo endelevu za uzalishaji
mali ikiwemo ukataji holela wa miti, uvuvi haramu, uzalishaji na utupaji
holela wa taka zimechangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa ardhi,
ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi, pamoja na upotevu wa bioanuai
na makazi.
Maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila kutunza
mazingira, ingawa jitihada kubwa za utunzaji wa mazingira zimefanyika
hali ya mazingira nchini bado si ya kuridhisha na imekuwa tishio kwa
mustakabali wa Taifa letu.
Shughuli ya uhifadhi wa mazingira inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo teknolojia ya uhandisi jeni, viumbe
wageni/vamizi, biofueli, na taka za kielektroniki, pamoja na ukosefu
wa wataalam wa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira,
Sura 191 katika ngazi zote.
Kutokana na Tanzania kukabiliwa na tishio la kuenea
kwa hali ya jangwa na ukame, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
inaratibu maandalizi ya Programu ya Kitaifa yenye madhumuni ya kufanya
tathmini ya maeneo yaliyoathirika ili kuweka malengo ya kuzuia uharibifu
wa ardhi ifikapo mwaka 2030.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya mwaka
2018/19, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,
January Makamba anasema Ofisi yake kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi
na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Iimeendelea kusimamia na kutekeleza
shughuli za uzingatiaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191
na Kanuni zake.
Makamba anasema NEMC imekuwa likishiriki katika hatua
zote muhimu za utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa kama vile, mradi
wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge na
mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi na kushirikiana na wawekezaji katika
sekta muhimu za kiuchumi ili kuhakikisha kuwa miradi yao inafuatiliwa
kwa karibu na kupata hati kwa muda mfupi.
Anaongeza kuwa katika mwaka 2017/18, NEMC ilifanya ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi 627 katika mikoa 23 nchini
ikiwemo Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Pwani, Morogoro, Kigoma, Tabora,
Dar es Salaam, Tanga.
Anaitaja mikoa mingine kuwa ni pamoja na Geita, Mwanza,
Dodoma, Songwe, Iringa, Lindi, Kagera, Mbeya, Ruvuma, Singida, Mara,
Shinyanga, Simiyu na Mtwara, ambapo NEMC imeshughulikia malalamiko 207
ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira kutoka kwa wananchi.
Waziri Makamba anasema katika kipindi cha mwaka 2017/18, Baraza kwa kushirikiana
na Chuo cha Madini na Halmashauri za Wilaya husika katika mikoa ya Geita
na Shinyanga limefanya tathmini kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ili
kuhakiki iwapo wanazingatia Sheria na Kanuni zake.
“Tathmini hii ilihusisha wachimbaji wadogo wanaotumia
Zebaki na wachenjuaji wanaotumia Sayanaidi (Cyanide) na katika mwaka
2018/19, Baraza litaendelea litaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo
na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kutatua changamoto zilizobainika
katika tathmini hiyo” anasema Waziri Makamba.
Anaongeza kuwa katika kuimarisha uzingatiaji wa Sheria ya Usimamizi wa
Mazingira, Ofisi yake imeteua wakaguzi 512 kutoka katika taasisi za
Umma na Serikali za Mitaa pamoja na kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa mazingira
128 kwa ajili ya kuongeza uwezo wa Serikali
kusimamia hifadhi ya mazingira.
Kwa mujibu wa Waziri Makamba anasema NEMC limesimamia uteketezaji wa taka hatarishi kutoka katika Vyuo Vikuu,
Viwanda, Magereza, Migodi, Viwanja vya Ndege na Maduka ya Madawa, ambapo
imeteketeza madawa chakavu yenye uzito wa tani 244.617 na lita 97 kwenye
mtambo wa Tindwa Incinerator, Mgodi
wa Buzwagi, Hospitali ya Muhimbili (Kampasi ya Mloganzila) na Safe Waste Incinerator
ya Mkuranga.
Kuhusu Tathmini ya Athari za Mazingira (TAM), anasema
katika mwaka 2017/18 Baraza limesajili jumla ya miradi 1,176 kwa
ajili ya kufanyiwa mchakato wa kupata
hati za TAM na miradi 533 imepewa vyeti kati ya miradi iliyosajiliwa.
“Hadi kufikia Desemba 2017, NEMC imesajili wataalamu
elekezi wa TAM 757, Wakaguzi wa Mazingira 357, Kampuni za Ushauri
wa TAM 152 na za Ukaguzi wa Mazingira 74 na kukamilisha maandalizi ya
Mfumo wa kuchakata TAM kwa njia ya mtandao” Anasema Waziri Makamba.
Waziri Makamba anasema kutokana na na malalamiko
ya wawekezaji kucheleweshewa kupata cheti cha TAM, NEMC imechukua hatua
mbalimbali ikiwemo Kupunguza gharama za TAM, Kutoa vibali vya muda (kwa
miradi ya viwanda pamoja na Kutengeneza orodha ya mambo muhimu ya kuzingatia
ya miradi ya majengo chini ya ghorofa tatu, viwanda na umeme jua.
Usimamizi wa Sheria ya Mazingira, Sura Na. 191 inapaswa
kutekelezwa ili kuweka mtazamo mpya katika namna bora ya kuchakata taka
ikiwemo ukusanyaji na usafirishaji wa taka na kuzitumia
kama malighafi ya kutengenezea mbolea, uzalishaji wa nishati ya umeme
na utengenezaji wa madampo ya kisasa.
Post a Comment