WANANCHI MWASUBUYA SIMIYU KUBADILI MAISHA YAO KIUCHUMI KUPITIA KILIMO CHA UMWAGILIAJI
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka akiteta jambo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Enock Yakobo(kushoto), katika hafla ya makabidhiano ya zana bora za
kilimo kutoka Kampuni ya Agricom Africa na Wakulima walio katika Mradi
wa Umwagiliaji , Septemba 03, 2018 katika Kijiji cha Mwasubuya.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na
wananchi wa Mwasubuya akiwa katika Moja ya Zana ya kupandia mpunga
ambayo ni miongoni mwa zana zilizokabidhiwa kwa ajili ya kuwawezesha
wakulima wa mradi wa Umwagiliaji wa Mwasubuya wilayani Bariadi, Septemba
03, 2018 katika Kijiji cha Mwasubuya.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Wananchi wa
Kijiji cha Mwasubuya wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu wamesema Mradi wa
Umwagiliaji wa Mwasubuya wenye ekari 514 utawasaidia kubadili maisha yao
kiuchumi kwa kuwa wanatarajia kuongeza mavuno kutokana na kuanza
kutumia zana za kilimo za kisasa katika uzalishaji kuanzia hatua ya
kuandaa mashamba hadi kuvuna.
Wananchi hao
wameyasema hayo baada ya makabidhiano ya zana za kilimo za kisasa
zitakazotumika kuanzia hatua ya kuandaa mashamba mpaka kuvuna, kutoka
Kampuni ya Agricom kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ambayo
imewadhamini wananchi walio katika mradi wa Umwagiliaji wa Mwasubuya,
yaliyofanyika katika eneo la Mradi Kijiji cha Mwasubuya, Septemba 03,
2018.
Wamesema pamoja
na kuongeza uzalishaji kutokana na uwepo wa maji ya uhakika ya Bwawa la
Mwasubuya na matumizi ya zana bora, mradi huo ambao utajikita zaidi
katika kilimo cha mpunga pia utawawezesha wananchi na hasa vijana
kujiajiri kupitia kilimo cha mboga mboga, hatimaye kukuza kipato chao na
Taifa kwa ujumla.
“Tumefurahi sana
kupata mradi wa umwagiliaji, hii ni ajira kwetu hasa sisi vijana wenye
nguvu, nina imani tukiutumia mradi huu vizuri utatubadilisha sisi
kiuchumi kwa sababu mashine za kisasa tulizoletewa tutazitumia kulima
eneo kubwa kwa muda mfupi, tutatongeza mavuno na kupata hela nyingi ”
alisema Daniel Ntobi Mkulima wa Mwasubuya
“Nimeupokea mradi
huu kwa furaha kabisa na nina uhakika kupitia mradi huu tutalima na
kupata mazao mengi hatutakuwa na njaa lakini pia mazao mengine tutauza
ili tujenge nyumba nzuri, tusomeshe watoto hata kijiji chetu
kitabadilika, cha msingi hapa tuutumie vizuri” alisema Monica Severine
Mkulima kutoka kijiji cha Mwasubuya
Naye Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhandisi. Wilbert
Siogopi amesema zana za kilimo zilizokabidhiwa na Kampuni ya Agricom
zitawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga na hivyo
kuongeza pato la kaya zao na kukuza uchumi wa Halmashauri na Taifa kwa
ujumla.
Kwa upande wake
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema dhamira ya Serikali
ni kuufanya Mradi wa Umwagiliaji Mwasubuya kuwa wa mfano ambao watu
kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakuja kujifunza, ambapo amebainisha
kuwa mpunga utakaolimwa utakuwa wa aina moja,utalimwa mara mbili kwa
mwaka na hautatumia mbolea za viwandani.
Ameongeza kuwa
pamoja na kilimo cha mpunga, Serikali mkoani humo imekusudia kufunga
kinu cha kukoboa mpunga na kupanga madaraja ya mchele na kupitia mradi
huo pia kutakuwa na ufugaji wa samaki katika Bwawa la Mwasubuya ambapo
vifaranga vitawekwa na ufugaji kupitia vizimba utafanyika sambamba na
kufuga samaki katika baadhi ya mashamba ya mpunga.
“Kwenye bwawa mle
tutaweka vifaranga vya sangara, kambare na sato pia katika ekari
zitakazolimwa ekari 10 zitatengwa ambazo mkulima atalima mpunga na
kufuga samaki kwa wakati mmoja, wakati akivuna mpunga anavuna na samaki;
tunataka kufunga kinu cha kukoboa mpunga na kupanga madaraja, nawaambia
maisha yenu yatabadilika, hapa ni mahali tunataka kuiambia dunia Simiyu
ni nini” alisema Mtaka.
Akizungumzia
namna wakulima watakavyolipa deni la mkopo wa zana bora za kilimo kutoka
Agricom, Mtaka amesema Halmashauri italima shamba lote ekari 514,
itatoa mbegu kwa wakulima, itapanda na kuvuna na baadaye itachukua
sehemu ya mavuno(gunia 10 kwa ekari) kutoka katika matarajio ya mavuno
ya kati ya gunia 30 hadi 42 kwa ekari, ili kufidia gharama za
uzalishaji na kurejesha deni.
Naye Mkurugenzi
wa Kampuni ya Agricom, Bi Angelina Ngalula amesema kampuni hiyo inafanya
kazi na Halmashauri na wakulima walio tayari na kubainisha kuwa
imekopesha Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mashine za kulimia, kupandia
na kuvunia zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 ambazo kwa
mujibu wa makubaliano zitalipwa baada ya mavuno.
Mradi wa
Umwagiliaji wa Mwasubuya una eneo lenye ukubwa wa ekari 700 zinazofaa
kwa kilimo cha umwagiliaji na umesajiliwa kwa Jina la Umoja wa
Umwagiliaji Mwasubuya (UMWASU) wenye wanachama 198.
Post a Comment