TRA YATOA ELIMU YA MAADILI, MABADILIKO YA SHERIA ZA KODI KWA WATUMISHI WAKE TANGA
Mwambawahabari

Meneja
wa Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Makao Makuu akiwasilisha mada kuhusu mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa watumishi
wa TRA mkoani Tanga kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao ili waweze
kutekeleza na kusimamia sheria za kodi kwa ufanisi na kutoa huduma stahiki kwa
wateja.
Na
Veronica Kazimoto
Tanga
Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) imetoa elimu ya maadili na mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa watumishi
wake mkoani Tanga kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao ili waweze
kutekeleza na kusimamia sheria za kodi kwa ufanisi na kufuata maadili ya kazi
ipasavyo.
Akizungumza wakati
akiwasilisha mada ya Mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya Mwaka 2018, Meneja wa
Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla kutoka TRA Makao Makuu amesema kuwa, kila
mtumishi wa TRA anapaswa kujua sheria za kodi na mabadiliko yake kwa undani ili
aweze kutoa huduma stahiki kwa wateja.
"Kila mwaka wa fedha unapoingia,
Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hufanya mabadiliko
mbalimbali ya sheria na kanuni za ukusanyaji wa kodi, hivyo ni muhimu kila
mtumishi wa TRA kujua mabadiliko na kanuni hizo kwa lengo la kutoa huduma
stahiki kwa wateja wetu," alisema
Masalla.
Aidha, Meneja huyo wa Elimu
kwa Mlipakodi amewataka watumishi hao kufuata sheria na kuepuka upendeleo
wakati wote wanapotoa huduma kwa wateja wanaotembelea ofisi za TRA.
Naye, Afisa Maadili
Mwandamizi Adelaida Rweikiza kutoka TRA Makao Makuu, amewaambia watumishi hao
kuwa, ni muhimu kuzingatia maadili kila wanapotimiza wajibu wao ili kuondoa
malalamiko ambayo yanaharibu taswira nzuri ya TRA.
"Kila mmoja wetu ana jukumu
la kuilinda taswira ya mamlaka yetu, hivyo ni wajibu wetu kuzingatia maadili ikiwa
ni pamoja na kutumia lugha nzuri kila tunapowahudumia wateja," alisema
Rweikiza.
Timu ya Maofisa wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania inaendelea kutoa elimu ya maadili na mabadiliko ya Sheria za
Kodi ikiwa ni pamoja na Msamaha wa Riba na Adhabu ya Malimbikizo ya Madeni ya
Kodi kwa watumishi wa TRA na wafanyabiashara wa Mikoa ya Kanda ya Kasikazini.
Post a Comment