Ads

KOCHA TAIFA STARS ATOA YAMOYONI

Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Emmanuel Amunike amesema kutimuliwa kwa wachezaji wa Simba na Yanga kwenye kikosi hicho huenda kumetokana na baadhi yao kutopata taarifa sahihi.
Akizungumza baada ya mazoezi ya kikosi hicho yanayofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani, Amunike alisema licha ya kuondolewa, wataendelea kuwa sehemu ya wachezaji wao kwa kuwa timu ya taifa ni ya watu wote. 
Walioondolewa juzi kutokana na kuchelewa kuripoti kambini katika muda uliotakiwa ni Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga, John Bocco, Jonas Mkude wote wa Simba na Feisal Abdallah wa Yanga.
“Kilichofanyika ni maamuzi ya timu na sio kwa maslahi ya mtu mmoja mmoja, wachezaji hao walikuwa sehemu yetu na wataendelea kuwa wachezaji wetu,” alisema.
 Amunike alisema mchezaji anastahili kupata nafasi kama anafanya vizuri, lakini kufanikiwa kwenye maisha ni lazima kuwepo na nidhamu na heshima na hilo ndilo jambo la msingi.
Nafasi za walioondolewa zilichukuliwa na Ally Sonso, Paul Ngalema wa Lipuli FC ya Iringa, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons ya Mbeya, David Mwantika, viungo Frank Domayo wa Azam FC, Salum Kihimbwa na mshambuliaji Kelvin Sabato, wote wa Mtibwa Sugar.
 Kuhusu mchezo dhidi ya Uganda alisema wanajiandaa vizuri wakijua wazi timu wanayokwenda kucheza nayo sio nyepesi. Alisema, Uganda itacheza kwa kujiamini kwa kuwa tayari ina pointi tatu ilizopata katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Cape Verde kwa hiyo wanaweza kucheza kwa kujiamini. 
Mechi hiyo ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika inatarajiwa kuchezwa Septemba 8, mwaka huu nchini Uganda.

No comments