MFUMUO WA BEI WAPUNGUA
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
MWAMBA WA HABARI
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam
Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Juni mwaka
huu umepungua kutoka asilimia 3.6 hadi kufikia asilimia 3.4.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), amesema
kuwa hali hiyo inatokana na kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa
mwaka ulioishia mwezi Juni mwaka huu kupungua ikilinganisha na kasi ilivyokuwa
kwa mwaka ulioishia mwezi Mei mwaka huu.
"Kupungua kwa mfumuko wa
bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni mwaka huu kumechangiwa na kupungua kwa
mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa
zisizo za vyakula" amesema Kwasigabo.
Amefafanua kuwa baadhi ya
bidhaa hizo zisizo za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei
ni bia asilimia 1.1, gharama za ukarabati wa vifaa vya umeme na
viyoyozi kwa asilimia 1.8, gesi za kupikia majumbani kwa asilimia 5.6.
Bidhaa nyengine zilizochangia
ni majiko ya mkaa kwa asilimia 2, gharama za mawasiliano kwa asilimia 2.6.
Kwasigabo ameeleza kuwa mfumuko wa bei
kwa baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki ikiwemo nchini Uganda kwa mwezi Juni mwaka umeongezeka na kufikia asilimia 2.2 kutoka asilimia 1.7.
Kwa upande wa kenya mfumuko wa bei umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.28 kutoka asilimia 3.95 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei mwaka huu.
Post a Comment