Manispaa ya Temeke wahamishia huduma zote za biashara Sabasaba
Mwambawahabari
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, imehamishia huduma zake za biashara katika Maonyesho 42 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, yanayoendelea kwenye Viwanja vya Maonyesho ya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwamba wa habari, kwenye banda la manispaa hiyo lililopo ndani ya ukumbi wa wa Benjamin Mkapa , kwenye viwanja hivyo, Msemaji wa Halmashauri hiyo, Eddah Mmali, amesema, nia ni kuwasogezea karibu huduma wananchi watakaofika katika viwanja hivyo vya maonyesho.
“Huduma zote za kibiashara zitapatikana hapa, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wanaoomba leseni kwa mara ya kwanza watapata leseni hizo, waombaji ambao walikwisha kuwa na leseni za biashara na kuisha muda wake yaani wanaohitaji kuhuisha leseni zao watapata huduma,”amesema Eddah.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano , chini ya Rais Dk. John Magufuli, imesisitiza ukusanyaji mapato hivyo kuna umuhimu mkubwa wa wafanyabiashara kuwa na leseni ili kukusanya mapato hayo.
“Ukiwa na leseni ya biashara inaepusha usumbufu wa kufuatiliwa kila mara katika biashara yako .Pia inaepusha faini au adhabu kubwa ambayo inaweza kutolewa kwa mujibu wa sheria.Wito wetu kwa wafanyabiashara wafike katika banda letu ili waweze kupewa hata elimu ya namna bora ya kuendesha biashara zao kwa mujibu wa sheria,”amesema Eddah.
Post a Comment