WANANCHI MKOANI NJOMBE WAITIKIA KWA WINGI KAMPENI YA ELIMU, HUDUMA NA USAJILI WA WALIPAKODI WAPYA
Mwamba wa habari
Na Mariam Mwayela Njombe
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutoa huduma, elimu na kusajili walipakodi
wapya katika maeneo ya Ludewa, Matamba, Ilembula, Mlangali, Ikonda na Makete
Mkoani Njombe ambapo mpaka sasa jumla ya walipakodi 351 wamesajiliwa.
Zoezi
hili limekuwa na muitikio mkubwa kutoka kwa wananchi ambao kwa muda mrefu
wamekuwa na shauku ya kupatiwa elimu ya kodi na kupata Namba ya Utambulisho wa
Mlipakodi (TIN).
Akizungumza
wakati wa kampeni hiyo Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Bw. Richard
Kayombo amewashukuru wakazi wa maeneo hayo kwa kuitikia wito na kuonyesha
shauku ya kutaka kujua mambo mbalimbali yanayohusu kodi hususani usajili wa
biashara, kuhakiki TIN na kusajili walipakodi wapya.
“Tunashukuru
sana kwa muitikio huu ulioonyeshwa katika zoezi hili hapa mkoani Njombe ambao unaonyesha uzalendo wa kuchangia mapato ya Serikali
kwa kujisajili na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi ambayo ni mwanzo
wa kutimiza wajibu wa kulipa kodi”, Alisema Kayombo.
Kayombo
amewaambia wafanyabiashara waliofika katika kampeni hiyo, kuwa na ukaribu na
maafisa wa TRA ili kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali katika kila hatua ya
ulipaji wa kodi na kutoa maoni yao ambayo yataboresha huduma zitolewazo na
Mamlaka.
Aidha,
Kayombo aliwakumbusha kulipa kodi sahihi na kwa wakati ili kuepuka faini na
adhabu zinazoambatana na ucheleweshaji huo. Vilevile, aliwasisitiza umuhimu wa
kutunza kumbukumbu sahihi za biashara, kutoa risiti pindi wanapouza bidhaa au
huduma na kudai risiti kila wanapofanya manunuzi mbalimbali.
Naye
William Kabupa ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wa duka la Nguo eneo la Ilembula,
ameishukuru TRA na kusisitiza kuwa, zoezi hili ni zuri na litasaidia
wafanyabiashara kutokuwa na sababu ya kukosa TIN au kukataa kulipa kodi.
“Nimefurahi
sana kupata TIN yangu leo hapa Ilembula kwani ilikuwa inanibidi kusafiri kwenda
Njombe mjini kupata TIN. Aidha, nashauri wafanyabiashara wenzangu wa Ilembula
wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata elimu na kusajiliwa ili waweze kulipa
kodi na kujivunia kuwa mmoja wa wachangiaji wa mapato ya Serikali” alisema
Kabupa.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania inaendelea na kampeni ya kutoa Elimu, Huduma na kusajili
walipakodi wapya Mkoani Njombe ambapo hadi sasa Walipakodi wa Wilaya za Makete,
Ludewa, Wanging’ombe na Njombe wanaendelea kupata huduma, elimu na kupatiwa
Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
Post a Comment