DKT TIZEBA ATOA SIKU 4 WAKULIMA WA MKONGE MKOANI TANGA KULIPWA FEDHA ZAO
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba akitoa maelekezo ya serikali wakati wa kikao cha pamoja na wadau wa Kilimo cha Mkonge cha mkataba (SISO) kabla ya mkutano wa wadau wa zao la Mkonge Uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jana 21 Juni 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe Martin Shigela akizungumza jambo kabla ya kumaribisha mgeni rasmi Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba kuongoza mkutano wa wadau wa zao la Mkonge Uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jana 21 Juni 2018.
Viongozi mbalimbali Mkoani Tanga wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe Martin Shigela wakiagana na Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa wadau wa zao la Mkonge Uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jana 21 Juni 2018.
Wadau wa zao la Mkonge wakichangia mada wakati wa mkutano wa wadau wa zao la Mkonge Uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jana 21 Juni 2018.
Na Mathias Canal-WK, Tanga
Wakulima wa Mkonge Mkoani Tanga wamempongeza Waziri wa Kilimo
Mhe Dkt. Charles Tizeba kupitia agizo lake alilolitoa kwa Kampuni ya Katani
Limited kuhusu kulipa madeni ya wakulima ndani ya siku nne kuanzia 21 Juni 2018
hadi 26 Juni 2018 Kwa madeni ya muda mrefu ya wakulima wa zao hilo jambo
lililopelekea kupunguza ufanisi na tija ya Kilimo Kwa wakulima hao.
Dkt Tizeba ametoa agizo hilo leo 21 Juni 2018 akiwa kwenye
mkutano na wadau wa Kilimo cha Mkonge cha mkataba (SISO) unaotekelezwa kwenye
mashamba matano ya Hale, Magunga, Magoma, Mwelya na Ngombezi yaliyo chini ya
miliki ya Bodi ya Mkonge Tanzania.
Katika Mkutano huu uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa
mkoa wa Tanga na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Martin Shigela sambamba na
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe Godwin Gondwe, Msajili wa Hazina, Mtendaji wa
BRELA, Muwakilishi wa mwanasheria Mkuu wa serikali, Mkurugenzi wa Bodi ya
Mkonge na wataalamu wengine; Waziri wa Kilimo Mhe Tizeba ametoa agizo hilo Kwa
Uongozi wa mfumo wa Kilimo cha wakulima wadogo wa kilimo cha Mkonge cha mkataba
(SISO), Kampuni ya Katani ltd ambayo ndio mnunuzi pekee wa Mkonge wa mkulima na
Bodi ya Mkonge Tanzania.
Sambamba na agizo hilo pia Mhe Waziri ameiagiza Bodi ya Mkonge
Tanzania kupitia upya mikataba yote iliyopo Kwa kushirikisha Bodi yenyewe,
Kampuni ya Katani na wadau wa zao hilo haraka iwezekanavyo ili kurekebisha
makosa yaliyopo.
Aidha, ameitaka Bodi hiyo ya Mkonge Tanzania kuitisha kikao na
wadau wote wa zao hilo ili kupitia upya utaratibu wa makato ya mgawanyo wa
mapato katika kusindika zao la Mkonge.
Mhe Dkt Tizeba aliongeza kuwa hati za miliki ya mashamba
zitapaswa kutolewa Kwa wahusika Mara baada ya kujiridhisha na mchakato
utakapokamilika huku akiwataka wakulima kulipa malimbikizo ya kodi ya ardhi.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba amemaliza ziara ya siku
moja ya kikazi mkoani Tanga huku akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe Martin
Shigela Kwa umakini na uwajibikaji katika kusimamia sekta ya Kilimo hususani
zao la Mkonge mkoani humo.
Post a Comment