KILIMO CHA PAMBA KUNOGESHA MAPINDUZI YA VIWANDA
*Ni kutokana na juhudi za Serikali za kuhamasisha kilimo cha pamba
ZAO
la pamba ni miongoni mwa mazao makubwa ya biashara yaliyokuwa
yakiliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni na kuchangia kukuza uchumi wa
wananchi miaka ya 1970.
Kwenye
miaka ya 1970 kulisheheni vyama vingi vya ushirika wa zao la Pamba na
viwanda vya kuchambua nyuzi na kukamua mafuta, ambavyo vilibadili hali
halisi ya kipato cha wananchi wa eneo linalolimwa zao hilo na kulifanya
kujulikana kama dhahabu nyeupe.
Kilimo
hicho kilianza kudorora miaka ya hivi karibuni kutokana na kulegalega
kwa vyama vya ushirika na matokeo yake pamba iliuzwa ikiwa chafu bila
kuzingatia ubora na madaraja yaliyopo.
Kutokana
na sababu hizo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John
Magufuli, iliamua kufufua zao hilo ili kuhakikisha upatikanaji wa
malighafi ya viwanda vya nguo na mafuta yatokanayo na mbegu za pamba
zinapatikana pamoja na kuinua uchumi wa wakulima nchini.
Katika
kufanikisha suala hilo Serikali ilianza kwa kuwaagiza viongozi wa mikoa
yote inayolima pamba kuhakikisha wanawahamasisha wakulima kufufua
mashamba yao na ilihakikisha inafuatilia jambo hilo kuanzia hatua za
awali za utayarishaji wa mashamba, ugawaji wa pembejeo hadi utafutaji wa
masoko.
Baada
ya kutoa agizo hilo ambalo lilifanyiwa kazi na tayari mafanikio
yameanza kuonekana katika msimu wa mwaka huu, kwa wakulima kuanza
kuvuna na kuuza kwa mafanikio.
Akizungumzia
kuhusu hali ya zao hilo mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John
Mongella, anasema msimu wa mwaka huu umekuwa na mafanikio makubwa
kutokana na hamasa iliyotolewa na viongozi wakuu wa Serikali.
Bw.
Mongella anasema kutokana na hamasa hiyo, mwaka huu wanatarajia kupata
mavuno makubwa kutoka katika kilimo hicho kwa sababu wakulima wengi
wamelima na baadhi yao tayari wameshaanza kuvuna.
Anasema
Rais Dk. Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, walitoa maelekezo
mahususi na walifanya ufuatiliaji wa karibu wa kilimo cha mazao makuu
matano ya biashara nchini, likiwamo na zao la pamba.
Akizungumza
kuhusu maendeleo ya zao hilo jijini Mwanza hivi karibuni, Bw. Mongella
amesema zao la pamba litasaidia kufufua viwanda vya mafuta ya kula, nguo
pamoja na kuongeza ajira.
Amesema
baada ya Rais Dkt. Magufuli kuhamasisha kilimo cha zao hilo, ambacho
kilianza kusuasua nchini, viongozi waliitikia na kuwahimiza wakulima
wachangamkie fursa hiyo, ambao walikubali.
“Tunashukuru
kwa hamasa na miongozo iliyotolewa na viongozi wetu kwa sababu
iliongeza ari kwa wakulima kulima zao la pamba kwa wingi na mwamko kwa
wananchi kulima mazao mengine, likiwamo la mpunga,” anasema.
Hata
hivyo, kiongozi huyo ameishukuru Serikali kwa kuagiza pamba
itakayovunwa iuzwe kupitia minada itakayosimamiwa na Chama cha Msingi
cha Ushirika (AMCOS) katika kila eneo, jambo ambalo limesaidia kufufuka
kwa vyama hivyo.
“Tunashukuru
kwa maelekezo na miongozo iliyokuwa inatolewa na viongozi wetu wakuu.
Sasa AMCOS zetu zimefufuka na huu ni mwanzo tu mapinduzi makubwa katika
biashara ya zao la pamba na yajayo yanafurahisha zaidi,” anasisitiza Bw.
Mongella.
Bw.
Mongella anatarajia kuwahamasisha wakulima wote wa mkoa huo pamoja na
wafugaji na wavuvi wajiunge katika AMCOS zilizoko katika maeneo yao, ili
kuweza kuirahisishia Serikali kufanyanao kazi.
Mkuu
huyo wa mkoa pia anatumia fursa hiyo kuwapongeza Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi wa Halmashauri, Maofisa Kilimo kuanzia ngazi ya wilaya hadi
kijiji na wakulima kwa kuhakikisha kilimo cha zao la pamba kinapata
mafanikio.
Bw.Mongella
anaamini ushirikiano wao kupitia vikosi kazi mbalimbali vilivyoundwa
kuanzia ngazi ya mkoa ambapo alikuwa Mwenyekiti watendaji hao walitoa
ushirikiano mkubwa ulichangia mafanikio ya zao hilo.
Hata
hivyo, Bw. Mongella amewashauri wakulima watumie taasisi za kifedha
kuhifadhi fedha zao na wajijengee nidhamu ya matumizi, ambayo itawapa
fursa ya kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo, ikiwa pamoja kujenga
nyumba bora.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza, Bw.
Juma Sweda anasema anaishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kulifufua
zao hilo pamoja na kuwahamasisha wananchi kulima na kutoa maelekezo ya
uuzwaji wake.
“Naishukuru
Serikali kwani baada ya kuwahamasisha ufufuaji wa kilimo cha zao la
pamba nasi tuliungana na wananchi kuhakikisha maelekezo hayo
tunayatekeleza kwa vitendo, lengo letu kubwa ni kuona zao hili linarudi
kama zamani.
‘’Mbali
na kuwahamasisha wananchi kulima zao la pamba, pia Watumishi wa
Halmashauri nao wamelima jumla ya ekari 306 za zao la pamba kwenye
kijiji cha Ikoma katika Kata ya Kijima. Mashamba yaliongeza hamasa kwa
wananchi,’’ anasema Sweda.
Bw.
Sweda anasema kabla ya wakulima kuanza kuanda mashamba ya kilimo cha
pamba, Wilaya ya Misungwi yenye vjjiji 113 ilitoa mafunzo kwa wakulima
wawili kila kijiji, ambao wameshirikiana na vikosi kazi vya vijiji
husika na Maafisa Ugani kusimamia kilimo cha zao hilo.
Anasema
kwa sasa wapo katika hatua ya uvunaji na uuzaji, ambapo wamejipanga
kukagua kikamilifu ili kuona zoezi hilo linaenda vizuri na pamba yote
inayopokelewa na vyama vya ushirika ni ile iliyo katika ubora
unaohitajika.
Anasema
baada ya Serikali kuhamasisha kilimo cha zao la pamba kwa mikoa yote
inayolima zao hilo, pia iliagiza kuanzishwa kwa Vyama vya Msingi vya
Ushirika (AMCOS) katika maeneo yote, ambapo AMCOS 50 zilianzishwa
wilayani Misungwi.
Bw.
Sweda anasema AMCOS zimesaidia kuimarisha ubora wa pamba, ambapo
viongozi wake hukagua pamba kabla ya kuipokea na iwapo mkulima
atabainika kupeleka pamba chafu hulazimika kuisafisha kwanza kwa kutenga
safi pembeni kabla ya kupima na kulipwa.
Mkuu
huyo wa Wilaya anaongeza kuwa, mbali na kukagua usafi na ubora wa pamba
ili kuhakikisha hakuna pamba chafu inayouzwa, pia wanasimamia zoezi la
malipo kwa wakulima na kwamba wanaouza wote wanalipwa hapo hapo na ni
marufuku mnunuzi kumkopa mkulima.
Pia,
anasema wilaya yao imeanzisha mikakati mbalimbali ya kutoa motisha kwa
Maafisa Kilimo na wakulima waliofanya vizuri, ambapo hutoa zawadi za
pikipiki kwa mkulima na afisa aliyeongoza katika kata yake.
Anaongeza
kuwa Maafisa Kilimo Wasaidizi wapo nchini Brazil kwa mafunzo ya miezi
mitatu, ambapo wanajifunza namna ya kilimo bora cha zao la pamba.
Viongozi hao ambao ni John Choto, Haika Kimambo na Bahati Mchele
walichaguliwa kuhudhuria mafunzo hayo baada ya kuonyesha jitihada kubwa
katika kusimamia zao hilo.
Mkuu
huyo wa wilaya anasema wilaya ina Maafisa Ugani 90 ambao wamesambazwa
kuanzia wilayani hadi vijiji, lengo likiwa ni kupata nafasi ya kusimamia
vizuri na kwa ukaribu zao la pamba.
Anasema
wilaya ina jumla ya kata 27 ambapo Maafisa Kilimo wake wote walipatiwa
pikipiki ili ziwawezeshe kuwafikia wakulima kwa urahisi na kuwahudumia
kwa wakati lakini atakayeshindwa kuwajibika atanyang’wanywa pikipiki.
Sambamba
na hayo, Bw. Sweda aliwashauri wakulima kutumia vizuri fedha
wanazozipata baada ya kuuza mazao yao. Anasema ni vema wakatumia fedha
hizo kujiletea maendeleo katika familia zao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
nyumba bora za kisasa na kuwaendeleza watoto wao kielimu.
Anasema
kwa sasa wapo katika hatua ya uvunaji na uuzaji, ambapo wamejipanga
kukagua kikamilifu ili kuona zoezi hilo linaenda vizuri na pamba yote
inayopokelewa na vyama vya Ushirika ni ile iliyo katika ubora
unaohitajika.
Anasema
viongozi wa Vyama vya Msingi vya AMCOS, hukagua pamba kabla ya kuipokea
na iwapo mkulima atabainika kupeleka pamba chafu hulazimika kuisafisha
kwanza kwa kutenga safi na chafu ndipo hupima na kulipwa.
Mkuu
huyo wa wilaya anaongeza kuwa zao la pamba mbali ya kuwapatia wakulima
kipato, pia litaimarisha hali ya usalama wa chakula kwa sababu fedha
watakayoipata baada ya kuuza pamba itawawezesha kumudu ununuzi wa
mahitaji mengine katika familia na hawatouza vyakula walivyonavyo.
Hata
hivyo, Bw. Sweda aliwaomba wadau wa sekta binafsi wasaidie katika
kuliongezea thamani zao hilo kwa kufanya uwekezaji mkubwa wa viwanda vya
nyuzi, nguo na vya kukamua mafuta ya pamba badala ya kuuza malighafi.
Kwa upande wake,
Afisa Kilimo wa Kata ya Mondo, Bw. Sebastian Mbandi anasema mafanikio
ya zao hilo kwa mwaka huu ni makubwa ukilinganisha na miaka iliyopita,
hata hivyo wameshindwa kufika lengo walilojiwekea kutokana na mazao
mengi kushambuliwa na wadudu aina ya thrips.
Bw.
Mbandi anasema walitarajia kuvuna wastani wa tani 1.5 kwa ekari moja
lakini kutokana na changamoto ya ugonjwa iliyosababishwa na mdudu huyo
wanatarajia kuvuna wastani wa kilo 800 kwa ekari hivyo ameiomba Serikali
kuwasaidia wakulima kwa kuwatafutia dawa itakayowawezesha kupambana na
thrips msimu ujao.
Kwa upande wao,
wakulima wakizungumza kwa nyakati tofauti, walitumia fursa hiyo
kumshukuru Rais Dk. Magufuli kwa kuhamasisha wananchi walime zao la
pamba, ambapo nao waliitikia wito huo na sasa wameanza kuona mafanikio.
Miongoni
mwa wakulima hao ni pamoja na Bw. Hoja Ngole mkazi wa Kijiji cha Mondo
ambaye amelima ekari sita na tayari ameshavuna na ameenda kuuza na
anatarajia kutumia fedha atakazozipata kwa kujenga nyumba ya kisasa.
Bw.
Ngole na mkewe Bibi Sara waliahidi kuongeza ukubwa wa shamba katika
msimu ujao na wamewaomba wananchi wengine kuchangamkia fursa ya kulima
zao hilo kwa kuwa ni mkombozi wa maisha yao. ’’Tumehamasika kuongeza
ukubwa wa shamba baada ya Waziri Mkuu kututembelea na tunataka akija
tena akute tumebadilika, tuwe na nyumba bora,’’ anasema.
Mkulima mwingine,mkazi
wa kijiji cha Mondo Bw. Michael Masalamunda ambaye alikuwa amepeleka
pamba yake katika kituo cha mauzo cha Mwanimo AMCOS amesema anatarajia
kutumia fedha atakazozipata baada ya mauzo hayo kwa kuongeza mtaji wa
biashara ya ng’ombe.
Bw.
Masalamunda naye amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuwahamasisha
walime zao la pamba pamoja na na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye naye
aliwahamasisha na kufuatilia maendeleo ya zao hilo.
Mkulima
huyo anaishukuru Serikali kwa kuagiza mauzo ya zao hilo yasimamiwe na
vyama vya ushirika kwa sababu vimewezesha wakulima kuwa na soko la
uhakika la pamba yao na wakiuza tu wanalipwa fedha zao hakuna
anayekopwa. “Mimi leo nakuja kuuza kwa awamu ya pili na fedha zote nimelipwa.”
Naye mkulima mwingine,
mkazi wa kijiji cha Maganzo Bw. Swalala Nteminyanda anaiomba Serikali
kuwatafutia dawa nzuri itakayoweza kuwaangamiza wadudu aina ya thrips
ambao wameonyesha usugu baada ya kupuliziwa dawa mbalimbali bila ya
kufa.
Nteminyanda
pia anawashauri wakulima wenzie wafuate maelekezo yanayotolewa na
Maafisa ugani wanaowatembelea katika mashamba yao ili waweze kupata
mavuno mengi na yenye viwango vya ubora vinavyotakiwa. Mkulima huyo
amelima ekari saba na anatarajia kujenga nyumba bora kwa fedha
atakazozipata.
Kwa upande waowanunuzi
wa zao hilo wanaishukuru Serikari kwa kuweka mfumo mzuri wa ununuzi wa
zao hilo, ambalo kwa mwaka huu linauzwa kupitia katika minada
inayosimamiwa na AMCOS.
Miongoni
mwa wanunuzi hao ni pamoja Meneja Mkuu wa Kampuni ya NGS Investment
LTD, Bw. Emmanuel Dandu alipokuwa akizungumzia kuhusu kuanza kwa
uchambuaji wa pamba kwa msimu wa mwaka huu.
Bw.
Dandu ambaye kampuni yao ya NGS Investment LTD, licha ya
kujishughulisha na biashara nyingine, pia inamiliki kiwanda cha
kuchambua pamba cha Majahida kilichopo wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu,
ambayo tayari imeshaanza zoezi ya uchambuaji pamba.
Anasema
pamba inayochambuliwa katika kiwanda hicho wanainunua kupitia AMCOS
walizopangiwa, ambapo alipongeza mfumo huo kwa sababu unawawezesha
kupata malighafi kwa urahisi na kwa wakati.
“Wanunuzi
wote tunanunua pamba kupitia AMCOS. Serikali imeweka mfumo mzuri
unaotuwezesha wote kununua pamba kadiri ya uwezo wetu. AMCOS zimeagizwa
kuuza pamba kwa wanunuzi wote bila ya ubaguzi, tofauti na miaka ya
nyuma” anasema Bw. Dandu.
Anasema
awali kabla pamba haijaanza kuuzwa kupitia AMCOS suala la ubora
lilikuwa halizingatiwi sana na wakulima kwani pamba yake ikikataliwa na
kampuni moja alikuwa na uhuru wa kuipeleka kwenye kampuni nyingine
jambo ambalo lilichangia kuishusha thamani.
Hata
hivyo, wanunuzi hao wanaiomba Serikali kuziwezesha AMCOS kuwa na
maghala makubwa na ya kisasa ya kuhifadhia pamba, lengo likiwa ni
kuhakikisha pamba inahifadhiwa kwenye maeneo salama na kuifanya
isipoteze ubora.
Mbali
na maombi hayo, pia wameiomba Serikali kuwajengea uwezo viongozi wa
Ushirika ili waweze kutekeleza majuku yao kikamilifu na pia isaidie
kutoa elimu kwa wanachama juu ya umuhimu na faida za AMCOS ili wakulima
wengi waweze kujiunga.
Akizungumzia
kuhusu uwezo wa kiwanda hicho, anasema kina uwezo wa kuchambua tani
40,000 za pamba kwa mwaka, lakini wanalazimika kuchambua wastani wa tani
tano hadi 12 kutokana na changamoto ya upatikanaji wa pamba ya kutosha
pamoja na changamoto ya umeme wa uhakika.
Pia
anaiomba Serikali iwasaidie wakulima kwa kuwapatia pembejeo kwa wakati
pamoja na kuwapa elimu ya mara kwa mara juu ya kulima kwa kufuata kanuni
bora za kilimo cha zao la pamba, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa wakati
ili waweze kujiongezea tija.
Anasema
kwa sasa kiwanda hicho kina jumla ya wafanyakazi 300, ambao kati yao 62
ni waajiriwa wa kudumu na waliosalia ni vibarua.
Bw.
Dandu anasema marobota yanayotengenezwa kiwandani hapo yanakuwa na
uzito wa kilo 200 hadi 220, huku wateja wao wakubwa ni Cotton
Distributors Inc (CDI) ya nchini Uswisi, Saurashtra Cotton and Agro
Product PVT LTD ya nchini India.
Wengine
ni Awatac Impex PTE LTD ya nchini Singapore pamoja na viwanda vya nguo
vya ndani ya nchi kikiwemo cha Mwatex cha jijini Mwanza. Alisema
matarajio ya kampuni hiyo ni kuanzisha kiwanda cha kutengeza nyuzi ili
kuongezea thamani ya pamba kabla ya kuiuza.
Aidha,
Meneja huyo anasema mbegu zinazopatikana baada ya pamba hiyo
kuchambuliwa zinapelekwa moja kwa moja katika kiwanda cha kukamua mafuta
ya kula na mashudu huuzwa kama chakula cha mifugo na mabaki
yanayopatikana baada ya mafuta kuchujwa, anasema yanatumika kwa
kutengeneza sabuni za kufulia, ambazo wanaziuza kwa wananchi.
Post a Comment