Balozi Ambokile kuzindua mgahawa wa chakula cha Kitanzania Afrika Kusini
Mwamba wa habari
BALOZI wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Sylvester Ambokile , anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mgahawa wa kisasa wa chakula cha Kitanzania uitwao Grill House Take Away jijini Johanesburg nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana kwa niaba ya Mmiliki wa Mgahawa huo , Christopher Robert, mwakilishi wa mkurugenzi huyo hapa nchini, Frank Koko alisema sherehe za ufunguzi rasmi zimepangwa kufanyika Juni 21 mwaka huu.
“Dhima yetu ni kukitangaza chakula asilia cha kitanzania kimataifa. Wapishi wote ni kutoka Tanzania na chakula kinasafirishwa kutoka Tanzania hadi nchini humo,”alisema Koko.
Alisema, kwa miaka mingi chakula cha kitanzania hakijapewa nafasi kubwa katika soko la hoteli na migahawa dunian kiasi cha kuwafanya hata watanzania wakiwa nje ya nchi kulazimika kula chakula ambacho si asili yao.
“Tuliona kwamba hata hoteli za kitanzania zinapika zaidi chakula cha utamaduni wa nje, watu wanalazimika kula tu.Ukifika Johanesburg ni changamoto kubwa kupata chakula cha nyumbani.
Watanzania wanahangaika kupata chakula cha asili yao jambo ambalo lilitusukuma kuja na wazo hili la kuwa na sehemu ambayo mtanzania akitua Johanesburg atapata huduma zote kama za nyumbani,”alisema.
Aliongeza; “ Tunaomba watanzania watakaotembelea Johanesburg watemelee Grill House Take Away , Mtaa wa 51 Regent ili waweze kutuunga mkono,”alisema Koko.
Post a Comment