Ads

BENKI YA TPB YAWATOA HOFU WATEJA WOTE WALIOKUWA BENKI YA TWIGA BANCORP.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mwamba wa habari
OFISA Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB Plc Sabasaba Moshingi amewatoa hofu wateja wote waliokuwa kwenye benki ya Twiga Bancorp huku akiwahakikishia kuwa wapo katika mikono salama na wataendelea kupata huduma kama hapo awali.


Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB Plc Sabasaba Moshingi akizungumza na wafanyakazi waliokuwa Twiga Bancorp pamoja na wateja wa benki hiyo jijini Dar es Salaam wakati anawakaribisha rasmi kutokana na Benki Kuu ya Tanzania(BoT),kuziunganisha benki hizo.



Moshingi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana baada ya benki ya TPB kuandaa hafla fupi ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuwakaribisha wateja na wafanyakazi waliokuwa kwenye benki ya Twiga Bancorp.

Kwa kukumbusha tu benki ya TPB na Twiga Bancorp zimeunganishwa Mei 17 mwaka huu baada ya Benki Kuu ya Tanzania(BoT) kutoa tamko rasmi.

"Hakuna kilichobadilika, huduma zitabaki pale pale, wateja wote mtaendelea kuhudumiwa katika matawi ya iliyokuwa benki ya Twiga Bancorp mpaka kipindi cha mpito kikimalizika.

"Kipindi cha mpito tulichopewa na BoT ni miezi mitatu, ambayo itatupa nafasi kuweka mitandao ya benki hizi pamoja na kurahisisha katika kutoa huduma za kibenki,"amesema Moshingi.

Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Windhoek Tanzania Simon Salatiel ambaye ni moja ya wateja wa iliyokuwa benki ya Twiga Bancorp akitoa shukrani zake jijini Dar es Salaam baada ya benki hiyo kuunganishwa na benki ya TPB Plc.
Kwa upande wake aliyekuwa Meneja Msimamizi wa iliyokuwa Benki ya Twiga Bancorp, Nkanwa Magina kutoka Benki Kuu ya Tanzania, amewataka wateja waliokuwa Benki ya Twiga Bancorp kutokuwa na wasiwasi, kwa kuwa kuunganishwa kwa benki hizo mbili kumeongeza nguvu katika utendaji wa kutoa huduma za kibenki.

Pia amesema wafanyakazi waliokuwa katika benki ya Twiga Bancorp, waendelee na moyo ule ule waliotoka nao kwenye benki yao na kuonesha ushirikiano wa dhati wa wafanyakazi pamoja na wateja wa benki ya TPB.

Wafanyakazi wa Benki ya TPB Plc(kulia), wakibadilishana mawasiliano baada ya benki hiyo kuwakaribisha rasmi waliokuwa wafanyakazi wa benki ya Twiga Bancorp ambapo kwa sasa zimeunganishwa.
Wakati huo huo waliokuwa wateja wa benki ya Twiga Bancorp, wametoa shukrani zao kwa uamuzi uliofanywa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kuunganisha benki hizo mbili, kwani ni faraja kwao na kusisitiza watapata huduma kwa ufanisi zaidi.

"Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Serikali ya Awamu ya tano kwa uamuzi huu waliouchukuwa wakuunganisha benki hizi mbili kwani umetuondolea wasiwasi sisi tuliokuwa wateja wa Twiga Bancorp,"amesema mteja aliyefahamika kwa jina la Janet Mmari.

Moja ya wateja wakubwa wa Benki ya Twiga Bancorp (kulia) akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya TPB Plc jijini Dar es Saalaam baada ya kufanyika hafla iliyoandaliwa na benki ya TPB kuwakarabisha wateja na wafanyakazi wa Twiga kutokana na uamuzi wa Benki  Kuu ya Tanzania(BoT)kuziunganisha benki hizo.Katikati ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB Plc Sabasaba Moshingi.

No comments