Ads

Vyombo vya Habari Vyaaswa Kuwa na Watumishi Wa kutosha Mkoani Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na watumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Kanda ya Kati Dodoma wakati wa ziara ya kutembelea vyombo vya Habari Mkoani Dodoma mapema leo.kulia ni Mkuu wa TBC Kanda ya Kati Bw. Bakari Msulwa

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA


Mkurugenzi wa Idara ya Habari Dkt. Hassan Abbas ametoa wito kwa vyombo vyote vya habari mkoani Dodoma na kwingine nchini kuhakikisha wanakuwa na wafanyakazi wa kutosha watakaokidhi mahitaji kutokana na Serikali kuhamia Dodoma.

Dkt. Abbas ametoa wito huo mjini Dodoma wakati wa muendelezo wa ziara yake kutembelea vyombo vya habari mkoani humo ambapo leo ametembelea ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Uhuru Redio pamoja na Uhuru gazeti.

“Lengo la ziara yangu ni kuona na kujua changamoto za kiutendaji mnazao kutana nazo pamoja na jinsi gani mmejipanga juu ya ujio wa Serikali kuhamia Dodoma kwani matukio mengi ya kiserikali yatafanyika Mkoani hapa” ameongeza Dkt. Abbas.Aidha, Dkt. Abbas amevitaka vyombo vya Habari kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano, ubunifu na kufuata maadili katika utendaji kazi hasa katika wakati huu wa mageuzi makubwa nchini.



“Katika mabadiliko au mageuzi yeyote hasa yanayoendelea sasa nchini kila mtu anapaswa kutimiza wajibu wake mahali pake pa kazi ili katika Tanzania ijayo ajivunie si kwa kuwa mlalamishi tu bali ajivunie kuwa naye alishiriki ipasavyo katika safari hii ya mabadiliko” amesisitiza Dkt. Abbas.



Dkt. Abbas ameongeza kuwa “Kwa upande wa habari mimi nimepewa jukumu la kusimamia maadili katika vyombo vya habari hivyo nasimamia na kufuata sheria na busara katika kila jambo linalohusu sekta ya habari ndio maana hatuchukui hatua tu bali tunashauriana na kuonyana kwanza pale wachache wanapokengeuka”.



Mbali na hayo Dkt. Abbas amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anapambana na azma ya kupigania nchi kujitegemea na si kutegemea nchi za nje kwa maisha yetu yote hivyo vyombo vya habari vinajukumu la kupongeza pale Serikali inapotimiza kazi vyema na kukosoa pale ambapo Serikali inakosea lakini si kwa kukejeli, kutusi au chombo cha habari kuonekana kinafanya inda.



Ziara hiyo itaendelea kesho mkoani humo ambapo Dkt. Abbas atatembelea vituo vya Redio Alternative Fm (AFm) na Redio Nyemo Fm.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akikagua vifaa vilivyopo ndani ya moja ya Studio za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Kanda ya Kati Dodoma wakati wa ziara yake mapema leo.

No comments