NI URA AU AZAM TENA BINGWA MAPINDUZI CUP 2017 LEO?
Mwambawahabari
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, Leo Jumamosi itakuwa kibaruani kutetea taji lake la
Kombe Mapinduzi, pale itakapokuwa ikipambana na URA ya Uganda kwenye
mchezo wa fainali utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar saa 2.15
usiku.
Mbali na kuwa mtihani wa kutetea
ubingwa walioutwaa mwaka jana kwa kuifunga Simba bao 1-0, Azam FC pia
itakuwa ikifukuzia rekodi mbili na kuweka historia mpya kwenye michuano
hiyo iliyoshirikisha timu 11 mwaka huu.
Rekodi ya kwanza ni ile ya kurudia
mafanikio waliyoyapata miaka mitano iliyopita walipolitwaa taji hilo
mara mbili mfululizo mwaka 2012 na 2013, hivyo wakilibeba tena kesho
itakuwa wamerudia mafanikio hayo kwani mwaka jana walilitwaa na mwaka
huu pia.
Mpaka sasa michuano hiyo ikiwa
katika mwaka wa 11, hakuna timu yoyote iliyolitwaa taji hilo mara mbili
mfululizo isipokuwa Azam FC iliyoweza kufanya hivyo.
Aidha rekodi ya pili, Azam FC
ikilitwaa taji hilo kesho kihistoria itakuwa ndio timu pekee iliyolitwaa
mara nyingi miongoni mwa timu zilizowahi kubeba kombe hilo, itakuwa
imefanya hivyo mara nne na kuizidi Simba ambayo imelitwaa mara tatu.
Azam FC imetinga fainali baada ya
kuichapa Singida United bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Shaaban
Idd, huku URA ikiitoa Yanga kwenye hatua ya nusu fainali kwa changamoto
ya mikwaju ya penalti 4-3 baada ya suluhu ndani ya dakika 90.
Akizungumza mara baada ya mazoezi
ya mwisho leo jioni, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, alisema
tayari wamemaliza kazi ya maandalizi ya mchezo huo huku akidai wachezaji
wako kwenye hali nzuri tayari kufanikisha ushindi muhimu kesho.
“Mara nyingi unapocheza na timu
ngumu unatengeneza mipango yako lakini inakuwa ni siri ya klabu kwa hiyo
hatuwezi kusema tunaingia na mbinu gani lakini URA tumeshacheza nao
zaidi ya mara moja na tunawajua, tumewaona walivyokuwa wakicheza mechi
za hapa na tunajipanga ni jinsi gani tutavunja nguvu zao na kutumia
udhaifu wao,” alisema.
Alisema timu hiyo kadiri
inavyoendelea kucheza mechi za michuano hiyo wanazidi kuimarika akidai
kuwa walivyoanza kucheza mechi za mwanzo ni tofauti na wanavyomalizia.
“Kwanza tunavijana wengi na wote
wako tayari kwa hiyo wanatupa hamasa kiasi kwamba kadiri unavyokwenda
hawaonyeshi kuchoka na wanaonyesha kupambana zaidi na kiwango kinazidi
kuongezeka kwa hiyo inatupa matumaini kutetea kombe letu,” alisema.
Akielezea siri ya mafanikio ya
kikosi hicho kuingia fainali mbili mfululizo, Cheche aliongeza kuwa:
“Siri ya mafanikio ni umoja na kukubaliana, wote tunaumoja,
tumekubaliana hii ni kazi yetu tuhakikishe tunaifanya vizuri na
tunaimalizia vizuri.”
Naye Nahodha wa timu hiyo, Himid
Mao ‘Ninja’, akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, alisema kuwa:
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kambi yetu iko vizuri, wachezaji wote wako
kwenye hali nzuri kila mtu nafikiri anatamani kupata nafasi ya
kuiwakilisha Azam FC na kuipatia matokeo.”
Mabingwa hao wanaodhaminiwa na
Maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents, wakitwaa
taji hilo watakuwa wamebeba kombe la kwanza msimu huu huku wakiwa kwenye
hatua nzuri ya kuyatwaa mengine mawili, lile la Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL) wakiwa wamelingana pointi na Simba kileleni kila
mmoja akiwa nazo 26.
Katika hatua nyingine, pia Azam FC
imetinga raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la FA (Azam Sports
Federation Cup) ikitarajia kukipiga na Shupavu FC ya Morogoro kati ya
Januari 31 au Februari Mosi mwaka huu, mchezo ukipigwa ugenini
Kilombero, Morogoro.
Post a Comment